1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yapanga kuendelea na mpango wake wa nyuklia.

16 Juni 2010

Rais Ahmadinejad asema Iran ndio itakuwa ikitoa masharti ya mazungumzo siku zijazo.

https://p.dw.com/p/NsYJ
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran atoa hotuba kwa taifa na kuzipuuza nchi za magharibi kuhusu mpango wake wa nyuklia.Picha: AP

Mkuu wa masuala ya nyuklia wa Iran, Ali Akbar Salehi amesema nchi hiyo inapanga kujenga kinu kipya cha nyuklia ambacho kitakuwa chenye nguvu zaidi kuliko kile cha utafiti kilichoko katika mji mkuu Tehran. Bw. Salehi amesema Iran itakuwa tayari na sehemu ya kwanza ya vipande vya nishati ya nyuklia vitakavyotumiwa katika kituo cha utafiti cha Tehran ifikapo Septemba mwaka ujao. Haya yanajiri wiki moja tu baada ya Iran kuwekewa vikwazo zaidi na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Mkuu huyo anayesimamia masuala ya nyuklia amesema Iran itatumia sera ya nipe-nikupe katika kukabiliana na mataifa yenye nguvu duniani ambayo yaliiwekea vikwazo vipya hata baada ya nchi hiyo kujitolea kujadili juu ya mpango wake wa nyuklia.

Salehi alisema mradi huo unaweza kuchukua miaka mitano na kwamba sehemu itakapojengwa haijaamuliwa na shirika la habari la ISNA limeinukulu ripoti inayokadiria kwamba kinu hicho kitatoa nishati ya Megawatti 20.

Bw Salehi alisema pia kwamba Iran inapania kujenga vinu kadhaa kote nchini humo ili iweze kuzalisha nishati kwa madhumuni ya mauzo katika nchi za kanda hiyo na mataifa ya Kiislamu yatakayoihitaji.

Tangu mwezi Oktoba, kituo cha utafiti kilichoko mjini Tehran kimekuwa chanzo cha mgogoro kati ya Iran na nchi za magharibi kutokana na usambazaji wake wa nishati.

Iran na nchi zenye ushawishi duniani zimeshindwa kupata muafaka kuhusu madini ya Uranium ambayo yakirutubishwa kuwa nishati yanakiendesha kituo hicho.

Mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani yamekuwa na hofu kuhusu madai ya kujipiga kifua ya Iran kwamba inaweza kutengeza vipande hivyo vya nishati lakini Bw. Salemi amesema Iran ina uwezo huo wa kitaalam.

Tangazo hilo ni hatua nyingine ya ukaidi wa Iran ambayo ilianza kurutubisha madini ya Uranium ya asilimia 20 kivyake licha ya kukosolewa vikali na nchi zenye ushawishi zilizoiwekea vikwazo wiki iliyopita. Mataifa hayo yanashuku kwamba Iran inatumia mpango wake wa nyuklia kuficha mpango wa kuundwa kwa bomu la nyuklia, madai ambayo Iran inayapinga.

Uamuzi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linasema kwamba lazima Iran iache mpango wake wa urutubishaji wa madini ya uranium.

Katika kikao cha bunge leo kilichojaa hamaki, Spika Ali Larijani alitoa wito kwa serikali ya Iran isonge mbele na urutubishaji wa viwango vya juu. Tovuti ya bunge hilo, limemnukuu Bw. Larijani akisema kwamba lazima nchi dhalimu zielewe kwamba shinikizo lao lisiloingia akilini litasawazishwa na kiwango cha Iran cha urutubishaji kitakachotegemea mahitaji yao.

Shirika la habari la IRNA limesema, wabunge wa Iran pia walipiga kura kuusoma kama jambo la umuhimu mkubwa, muswada utakaohakikisha serikali inaendelea na kazi ya urutubishaji. Muswada huo pia utaipa serikali nguvu ya kuzuia wakaguzi kuingia Iran ikiwa watatoa habari kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran aidha kwa vyombo vya habari au nchi nyengine.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, leo aliikosoa sera ya nchi za magharibi akiapa kwamba Iran ndio itakuwa ikitoa masharti ya mazungumzo ya siku zijazo na kwamba wataweka masharti kuziadhibu. Katika hotuba yake iliyokuwa ya moja kwa moja kwa taifa, rais huyo alisema ikiwa haki za Iran zitakiukwa, ina haki ya kulipiza kisasi.

Mwandishi, Peter Moss / AFP

Mhariri, Josephat Charo