1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yapinga mabadiliko ya mkataba wa nyuklia

Caro Robi
14 Januari 2018

Iran inapinga mabadiliko yoyote katika mkataba uliofikiwa kati yake na nchi sita zenye nguvu zaidi duniani baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutaka hatua zaidi kuhakikisha mkataba huo unaendelea kutekelezwa.

https://p.dw.com/p/2qoVK
Mohammad Javad Zarif iranischer Außenminister
Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema haitakubalia marekebisho yoyote kufanyiwa mkataba huo sio sasa wala katika siku za usoni na haitakubali masuala mengine kuhusiswa na mkataba huo wa kinyuklia uliiofikiwa mwaka 2105 unaojulikana kama mpango wa utekelezaji wa pamoja JCPOA. Urusi imeionya Marekani kuwa kujiondoa kutoka mktaba huo itakuwa ni kosa kubwa.

Marekani yatilia shaka makubaliano

Makubaliano hayo yanayolenga kuidhibiti Iran kutoendeleza mipango yake ya kuunda silaha za kinyuklia na badala yake iondolewe baadhi ya vikwazo vya kiuchumi yanaungwa mkono na Urusi, Uingereza, Ufaransa, Urusi, Ujerumani na Umoja wa Ulaya isipokuwa tu Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump imekuwa ikitilia shaka utayari wake wa kuendelea kuwa sehemu ya nchi zilizotia saini makubaliano hayo ya JCPOA.

USA Trump erhöht den Druck auf den Iran
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture alliance/dpa/AP/E. Vucci

Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov amesema wanapata taarifa kuwa huenda uamuzi umeshafikiwa Marekanii wa kutaka kujiondoa kutoka mkataba huo wa kinyuklia au uamuzi huo uko karibu kufikiwa na kuongeza iwapo Marekani itachukua uamuzi huo, basi ifahamu kuwa itakuwa mojawapo ya makosa makubwa iliyochukua kuathiri sera za kigeni.

Mnamo siku ya Ijumaa, Trump aliahirisha utekelezaji wa baadhi vikwazo vinavyohusiana na uuzaji wa mafuta na mfumo wa benki wa Iran, akisema amechukuwa tu hatua hiyo ili kupata makubaliano na washirika wa Ulaya ili kurekebisha kasoro zilizomo katika makubaliano hayo.

Trump anataka makubaliano mapya ya kuudhibiti zaidi mpango wa kinyuklia w a Iran utakaojumuisha vikwazo zaidi vinavyolenga vinu vya kinyuklia vya Iran. Hata hivyo nchi nyingine zenye nguvu zaidi duniani zilizoshiriki katika mkataba wa 2015 zinasema makubaliano hayo yanafanya kazi kama ilivyotarajiwa na kuwa Iran inaheshimu na kutimiza yaliyofikiwa katika makubaliano hayo.

Macron asisitiza makubaliano yadumishwe

Siku ya Jumamosi (13.01.2018) Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisisita kuwepo haja ya pande zote zinazohusika kuheshimiana kuhusiana na mkataba huo kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani akitaka mkataba huo kudumishwa kama ulivyo. Aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu aliyoyafanya na Waziri mkuuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

China Staatsbesuch Emmanuel Macron | PK in der französichen Botschaft
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/C. Platiau

Hata hivyo Netanyahu, mkosoaji mkubwa wa makubaliano hayo amemueleza Rais huyo wa Ufaransa kuwa kufanyia marekebisho mkataba huo wa kinyuklia kutaongeza nafasi za kuhakikisha unadumishwa.

Iran inasema Marekani kuendelea kuiwekea vikwazo katika masuala ambayo si ya kinyuklia kama yanayohusiana na haki za binadamu na maaribio ya makombora kunaifanya nchi hiyo kushindwa kunufaika kifedha na kiuchumi kama ilivyotarajiwa baada ya kufikiwa makubaliano ya JCPOA.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif  amesema msimamo hasi wa Trump kuhusu makubaliano hayo na Iran kwa jumla pia umekiuka makubaliano ya kuepuka kuingilia moja kwa moja sera za Iran na hivyo kuhujumu kurejea katika hali ya kawaida kwa mahusiano ya kibiashara na kiuchumi na Iran.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Zainab Aziz