1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasubiri uamuzi wa Marekani kuhusu mkataba wa nyuklia

Lilian Mtono
8 Mei 2018

Rais Donald Trump wa Marekani anatarajiwa kutangaza iwapo ataachana na mkataba wa nyuklia wa Iran, huku rais wa Iran akionya kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kupitia kipindi kigumu kufuatia maamuzi yatakayotolewa na Trump

https://p.dw.com/p/2xLNR
Iran Hassan Rouhani
Picha: picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Rais Trump anatarajiwa kutangaza maamuzi hayo baadaye hii leo. Mkataba huo ambao ulifikiwa chini ya mtangulizi wake Barack Obama, kwa ushirikiano na China, Urusi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ulikuwa na lengo la kuleta nafuu ya vikwazo dhidi ya Iran, ambapo badala yake ilitakiwa kuachana na kile ambacho mataifa ya Magharibi yalihofia kuwa ilikuwa ni mipango ya silaha za nyuklia. 

Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter jana usiku kuhusiana na hatua hiyo.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani ameonya kuhusu uwezekano wa taifa hilo kupitia katika kipindi kigumu, baada ya maamuzi hayo. Bila ya kumtaja moja kwa moja Trump, matamshi ya Rouhani aliyoyatoa kwenye mkutano wa masuala ya mafuta mjini Tehran, yanawakilisha tamko rasmi la Iran, baada ya ujumbe huo wa Trump.

Rouhani ameongeza kuwa Iran inataka mahusiano yenye tija na ulimwengu, lakini itaendeleza maendeleo ya ndani licha ya vikwazo vinavyotarajiwa dhidi yake kutoka Marekani.  

USA Donald Trump erneuert Einreiseverbot
Trump anatishia kujiondoa katika mkataba wa IranPicha: picture-alliance/dpa/NOTIMEX/Casa Blanca

Mkuu wa benki kuu ya Iran Valiollah Seif amesema kupitia kituo cha televisheni cha serikali kwamba uchumi wa nchi hiyo hautaathirika kivyovyote iwapo rais Trump ataiondoa Marekani kwenye mkataba huo. Amesema wamejiandaa kwa lolote linaloweza kujitokeza.

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza katika wiki za hivi karibuni walifanya mazungumzo na Trump ya kumshawishi kutojiondoa kwenye mkataba huo, lakini rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema, uwezekano ni mkubwa kwamba juhudi zao zimeshindwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson hapo jana amesema kwa sasa hakuna mbadala unaofaa wa mkataba huo wa nyuklia, lakini pia mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Ufaransa wakiiomba Marekani kutojiondoa, ili kuepusha kile wanachoamini kwamba ni uwezekano wa kuongezeka kwa silaha, na kupunguza usalama duniani. Heiko Maas ni waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly, amesema kuudhoofisha mkataba huo wa nyuklia wa Iran huenda kukachochea hali kuwa mbaya zaidi katika ukanda huo ambao mara kwa mara hukabiliwa na mizozo.

Bei ya mafuta imeporomoka barani Asia baada ya kuwa juu kwa takriban miaka mitatu na nusu, wakati ambapo wawekezaji wakisubiri kwa hamu tangazo hilo la Trump.

Trump mara kwa mara ametishia kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba huo. Wakati wa kampeni ya urais za mwaka 2016, Trump alisema hakubaliani nao, na baada ya kuingia madarakani alitishia mara kadhaa kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo ambao wiki iliyopita alisema ni "mbaya zaidi".

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/DPAE/APE
Mhariri:Josephat Charo