1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yazusha taharuki duniani

Saumu Mwasimba
8 Julai 2019

Hatua ya kutangaza kukiuka mkataba wa Nyuklia wa 2015 na kuvuka viwango vya urutubishaji madini ya Urani imezusha wasiwasi kuanzia ulaya mpaka Marekani. Umoja wa Ulaya na Urusi zasema zina wasiwasi mkubwa

https://p.dw.com/p/3LlFV
Iran PK Regierungssprecher zu Atomabkommen
Picha: Irna

Iran imetangaza kupitia shirika lake la nguvu za atomiki kwamba itaongeza kiwango cha urutubishaji madini ya urani na kufikia asilimia 4.5. Tangazo hilo limezusha hisia kubwa kimataifa,ambapo mjini Brussels Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi mkubwa kutokana na mipango hiyo ya Iran inayokiuka makubaliano ya mwaka 2015.

Jumapili Iran ilitangaza kwamba itakiuka kipengele cha makubaliano ya Nyuklia cha ukomo wa kiwango cha urutubishaji madini ya Urani,katika kipindi cha masaa machache yajayo.Lakini Leo jumatatu nchi hiyo ikatangaza imeshavuka asilimia 3.5  ya viwango vya mwisho vinavyokubalika vya urutubishaji wa madini hayo na kufikia asilimia 4.5.

Onyo la Iran

Iran pia imezionya nchi za Ulaya dhidi ya kuchukua hatua yoyote ya kuujibu uamuzi wake huo wa kuukiuka mkataba wa mwaka 2015 ikisema ikiwa hilo litafanyika itaamua kuzivuka hatua zake zote nyingine walizopanga na kutekeleza hatua ya mwisho.Ingawa pia msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa nchi hiyo Abbas Mousavi hakufafanua juu ya hatua ya mwisho inayozungumziwa.

US Atomrakete
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Riedel

Fikra zote kwa mara nyingine hivi sasa zimeelekezwa katika kuangalia ni kwa jinsi gani Iran huenda ikawa inakaribia kutengeneza silaha za Nyuklia.Mousavi alipoulizwa na waandishi habari ikiwa Iran inaweza kujiondowa kabisa katika makubaliano ya kimataifa ya Nyuklia alijibu kwamba kila kitu kinawezekana ingawa hakuna uamuzi uliokwishafikiwa na nchi yake.

Ujerumani,Ufaransa na Uingereza  washirika pekee wa Ulaya waliobakia kuunga mkono mkataba huo wameitolea mwito serikali mjini Tehran kusitisha hatua yake ya kuelekea kuukiuka kabisa mkataba huo lakini Iran kwa upande mwingine inasema imepoteza subira na hali ya kushindwa kwa washirika hao wa Ulaya kuchukua hatua za kuisaidia kiuchumi kukabiliana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani vinavyoididimiza Iran.

Jibu la Ujerumani

Ujerumani imesema inataka kusubiri kuona ripoti ya uchunguzi itakayotolewa na shirika la kudhibiti  kuenea kwa teknolojia ya nyuklia duniani IAEA juu ya madai hayo ya Iran ya urutubishaji madini yake ya Urani kupindukia viwango vilivyowekwa chini ya mkataba wa mwaka 2015.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani Rainer Breul  amezungumza na vyombo vya habari leo na kusema

''Hatujibu matangazo yaliyotolewa. Tunajibu kile ambacho kitaripotiwa na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki kama ilivyowekwa katika makubaliano. Ni kutokana na sababu hii ndio maana kuna hatua zote hizi za uwazi na uangalizi. Sisi bado hatua ripoti ya IAEA inakuja. Siwezi kuwaambia ni lini,inategemea vitu mbali mbali. Hata hivyo tunahakika kwamba IAEA itafanya hivyo haraka iwezekanavvyo.Kwahivyo ni suala na siku kadhaa na sio wiki.''

Roter Platz in Moskau
Picha: picture-alliance

Urusi kupitia msemaji wa ikulu ya Kremlin amesema nchi hioyo ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya Iran na Marekani kuhusiana na suala hilo la Nyuklia.Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari wanawsiwasi na tangazo la Iran lakini pia akasema serikali ya nchi yake iliwahi kuonya kwamba Uamuzi wa Trump wa kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa Nyuklia mwaka mmoja uliopita utakuwa na athari mbaya kwa usalama wa dunia. Urusi imezitolea mwito pande zote kutumia diplomasia kuondoka kwenye mgogoro huu. Hivi sasa Iran imetowa siku 60 kwa nchi zilizobakia kwenye mkataba huo ikiwemo Urusi kutafuta njia ya kuondowa makali ya vikwazo vya Marekani la sivyo ichukue hatua zaidi zilizoko nje ya makubaliano ya mwaka 2015.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sekione Kitojo