1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq na Marekani kuendelea na mashauriano kuhusu iwapo jeshi la Marekani liendelee kuhudumu nchini Iraq au la.

Ponda, Eric Kalume27 Oktoba 2008

Marekani na serikali ya Iraq zikijaribu kufikiana kuhusu mpango mpya wa kubakia kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq, nchi hiyo sasa imejikuta katika njia panda baina ya maslahi ya Marekani na vitisho vya Iran.

https://p.dw.com/p/FiL0
Mwanajeshi wa Marekani akishika doria nchini Iraq.Picha: AP


Huku Marekani na serikali ya Iraq zikijaribu kufikia maafikiano kuhusu mpango mpya wa kubakia kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq baada ya jeshi la muungano uliotolewa na Umoja wa mataifa nchini Iraq kumalizika tarehe 31 mwezi Disemba, Iraq sasa imejikuta katika njia panda kati ya matakwa ya Marekani na hofu inayotokana na vitisho vya Iran inayopinga kuendelea kuwepo kwa jeshi la Marekani katika ardhi hiyo ya Iraq.


Tangu uvamizi wa kijeshi wa mwaka wa 2003 uliongozwa na Marekani nchini Iraq, na hatimaye kumng´oa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Saddam Hussein, Iran imelichukulia taifa hilo linaloongoza na Wa-Shia wengi walio wengi, kuwa mshirika muhimu katika mvutano kati yake na serikali ya Marekani.


Aidha serikali hiyo ya Iran imekuwa ikijaribu kukita mizizi katika ushawishi wake wa masuala ya ndani ya Iraq bila ya mafanikio, kutokana na kuwepo kwa mkono wa Marekani katika siasa za nchi hiyo.


Serikali ya Rais Mahmoud Ahmadiejad nchini Iran imepinga vikali mashauri ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya serikali ya Iraq na Marekani tangu mwezi Februari mwaka huu, kuhusiana na utaratibu wa mpango wa kuyaondoa majeshi ya marekani katika ardhi ya Iraq.


Kulingana na ratiba ya kuondoka kwa majeshi ya kigeni nchini humo, majeshi ya Marekani yanatarajiwa kuanza kuondoka nchini Iraq mwaka ujao, baada ya kipindi cha kuhudumu kumalizika tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu.


Lakini Serikali ya Iraq na Marekani zimekuwa zikifanya mazungumzo ya kutaka kuongezwa kwa muda huo wa kuhudumu kwa jeshi la Marekani nchini hadi mwaka wa 2011, hatua inayopingwa vikali na Iran.


Msimamo wa Iran kwenye mashauriano hayo, umezua hofu miongoni mwa baraza la Mawaziri la nchini Iraq, ambalo sasa linataka mkataba huo ufanyiwe marekebisho, hatua ambayo pia inatajwa kuzua wasiwasi miongoni mwa maafisa wa kuu wa kisiasa na pia katika jeshi la Marekani,wakihoji kuwa huenda hatua hiyo ikawa na athari kubwa iwapo mkataba huo hautakamilishwa.


Marekani ambayo bado inakabiliana na makundi ya wapiganaji nchini Iraq,imemshtumu vikali rais Mahmoud Ahmadinejad kwa kujaribu kuvuruga mpango huo huku kwa upande wake Rais Ahmadinejad akiishtumu vikali serikali ya Marekani kwa kukiuka mpango wa umouja wa mataifa wa kuyaondoa majeshi ya kigeni kuanzia mwezi Disemba mwaka huu.


Iran ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilumbana na serikali ya Marekani kuhusiana na mpango wake wa Nuklia, inaamini kuwa kuendelea kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika taifa hilo jirani ni tisho kubwa kwa maslahi yake katika eneo la Mashariki ya kati.

Wiki iliyopita kulitokea mgawanyiko mkubwa katika baraza la mawaziri nchini Iraq, kuhusiana na iwapo mpango huo ufanyiwe marekebisho au la wakati viongozi kwenye mashauriano hayo watakapokutana tena wiki hii.

Waziri mmoja ambaye jina lake hakutaka litajwe, alieleza hofu yake kuwa iwapo mpango hzuo hautafanyiwa marekebisho huenda wakauawa mmoja baada ya mwengine.


Hata hivyo waziri wa Sayansi na Teknolojia nchini Iraq Raid Jahid Fahmi alisema kuwa watajaribu kupima mizani kati ya maslahi ya Marekani na tisho la Iran katika eneo hilo.


Endapo mkataba huo hautafanikishwa, litakuwa pigo kubwa kwa utawala wa Rais George Bush ambaye muda wake unafikia kikomo Januari mwakani.