1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yaimarisha mashambulio Mosul

John Juma
5 Januari 2017

Mapema leo operesheni ya kijeshi imefanywa kuanzia maeneo ya magharibi ya Anbar kulikomboa jimbo hilo kutoka mikono ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu-IS

https://p.dw.com/p/2VJwn
Irak US-Truppen in Mossul
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Jeshi la Iraq na vikosi vya usalama vimeimarisha vita dhidi ya wapiganaji wanaojiita Dola la Kiislamu katika juhudi za kuukomboa mji wa Mosul. Hayo ni kwa mujibu wa kamanda wa Marekani anayeongoza ushirikiano wa vikosi hivyo vya usalama ambavyo juhudi zao sasa zimeingia wiki ya 11.

Mapema leo operesheni ya kijeshi imefanywa kuanzia maeneo ya magharibi ya Anbar kulikomboa jimbo hilo kutoka mikono ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu-IS. Amesema Luteni Jenerali Qassem Mohammedi, kamanda wa operesheni za Jazeera.

Ameongeza kuwa maeneo makuu wanayoyalenga ni Aanah, Rawa na Al-Qaim, yaliyoko magharibi ya Iraq.

Tangu kurejelea mashambulio wiki iliyopita, vikosi maalum vya kupambana na ugaidi vile vya mashambulizi ya dharura na vya polisi, vimefaulu kudhibiti wilaya kadhaa za mashariki ya mji huo, licha ya upinzani mkali.

Luteni kanali Steve Townsend
Luteni kanali Steve TownsendPicha: Reuters/M. Al-Ramahi

Hayo ni kwa mujibu wa Luteni Jenerali Steve Townsend ambaye ameongeza kusema kuwa wiki mbili zilizopita, makamanda wa Iraq waliamua kuwa majeshi yanayoiunga mkono serikali yatashirikiana pamoja kuweka taratibu zao, utaratibu ambao haujawa mzuri katika miezi miwili iliyopita, hali ambayo imepunguza kasi ya juhudi za majeshi ya Iraq. Townsend amesema ''Tunaona mafanikio. Awali tulikuwa tukishuhudia ufanisi sehemu moja na mikwamo katika sehemu nyingine, lakini sasa tunasonga mbele katika nyanja zote mashariki ya Mosul.''

Kikosi maalum cha kukabiliana na ugaidi kiliingia Mosul na kudhibiti robo ya jiji hilo, lakini majeshi kwa upande wao yalikwama na kusababisha juhudi za kijeshi kusimama kwa mwezi uliopita.

Makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Iraq wanaendeleza mashambulio kuukomboa mji huo ambao ndio ngome kuu iliyosalia ya IS nchini humo. IS limepoteza nusu ya ngome iliyokuwa ikidhibiti zamani, na kupoteza udhibiti wa Mosul utakuwa pigo kubwa kwake

Kando na hayo, bomu lililotegwa kwenye gari limelipuka katika mji mkuu wa Iraq Baghdad na kusababisha vifo vya watu watano, na kuwajeruhi wengine saba. Shambulio hilo limetokea katika wilaya ya mashariki ya Abadi.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/DPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo