1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yazidi kudhibitiwa Iraq na Syria

Lilian Mtono
3 Novemba 2017

Vikosi vya Iraq vimeingia katika mji wa al-Qaim, moja ya maeneo yaliyokuwa yamesalia mikononi mwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Mafanikio kama hayo yanaripotiwa pia upande mwengine wa mpaka, yaani nchini Syria.

https://p.dw.com/p/2mxN1
Irak Region irakische Sicherheitskräfte
Picha: picture-alliance/AP/K. Mohammed

Vikosi vya Iraq vimefanikiwa kuingia katika mji wa al-Qaim, ambao ni moja ya maeneo yaliyokuwa yamesalia mikononi mwa kundi la wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu, IS. Mafanikio kama hayo dhidi ya IS yanaripotiwa pia upande mwengine wa mpaka, yaani nchini Syria. 

Vikosi kutoka jeshi la Iraqi, Kikosi Maalum ya Kupambana na Ugaidi, wanamgambo wa madhehebu ya Sunni na wale wa Kishia wanaoungwa mkono na Iran, wanashiriki kwenye mashambulizi ya kuikomboa miji ya al-Qaim na Rawa, miji miwili ambayo iko katika eneo la mpaka wa Iraq na Syria. Meja Generali Noman Abed al-Zobai, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi hivyo vimekwishaanza mashambulizi katikati ya mji wa Al-Qaim.

Mapema asubuhi ya leo, majeshi ya Iraqi yalianzisha mashambulizi ya ardhini kwenye maeneo walikokuwa wanamgambo hao yakisaidiwa na mashambulizi ya kutoka angani yanayofanywa na vikosi vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, alisema kwenye taarifa yake iliyotangaza kuhusu operesheni hiyo wiki iliyopita kwamba "wanamgambo wa IS wanatakiwa kuchagua ama kufa au kusalimu amri."

Syrien - russicher Militärhubschrauber fliegt über Palmyra
Wanajeshi washirika wanaounga mkono vikosi vya Syria katika operesheni ya kuwaondosha wapiganaji wa ISPicha: picture alliance/AP Photo

Mafanikio pia yaonekana nchini Syria.

Wakati huo huo, jeshi la Syria limetangaza leo hii kwamba limeukomboa mji ambao umepiganiwa kwa kipindi kirefu wa Deir el-Zour ulioko mashariki mwa nchi hiyo, kutoka kwa wanamgambo wa Dola la Kiislamu, hatua inayotajwa kama alama ya ushindi mkubwa katika operesheni za kijeshi za kukomboa ngome zilizosalia ambazo awali zilishikiliwa na kundi hilo katika jimbo lenye utajiri wa mafuta lililopo katika mpaka na Iraq.

Kwenye taarifa yake, jeshi la Syria limesema hivi sasa lina udhibiti kamili wa mji huo, baada ya kampeni ya wiki nzima iliyofanywa na vikosi vya washirika. Limesema vikosi maalumu vya jeshi hivi sasa vinaondoa mitego na mabomu ya kufukiwa ardhini yaliyotegwa na wanamgambo hao wenye itikadi kali katika mji huo.

Deir-el-Zour ilikuwa imegawika kwa takribani miaka mitatu, ambapo upande mmoja ulikuwa unashikiliwa na majeshi ya serikali na huku mwengine ukiwa chini ya utawala wa Dola la Kiislamu.

Majeshi ya serikali ya Syria kwa kushirikiana na majeshi washirika yanayounga mkono serikali hapo awali walifanikiwa kuliingia kwenye eneo lililokuwa limezingirwa na wanamgambo wa IS kwenye mji huo mnamo mwezi Septemba katika shambulizi lililopata usaidizi wa vikosi vya Urusi, na tangu hapo yamekuwa yakisonga mbele katika harakati za kuwafurusha wanamgambo hao.

Hatua hii ni ya hivi karibuni inayoonesha kushindwa kwa kundi hilo la IS, wakati wapiganaji hao wakishuhudia kunyang'anywa takriba ngome zote za mijini ambazo awali walijitangazia ukhalifa. 

Jeshi la Syria, linaloungwa mkono na Urusi na Iran, pamoja na vikosi vya Syria vinavyoongozwa na Wakurdi na kuungwa mkono na Marekani hivi sasa vinasonga mbele kuikomboa miji iliyosalia katika jimbo la mashariki lenye utajiri wa mafuta, ukiwemo mji muhimu wa Boukamal, uliopo karibu na mpaka wa Iraq.    

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef