1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad. Benazir kufanya mkutano na wanasiasa wa upinzani.

7 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C79I

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto yuko mjini Islamabad kwa mazungumzo na wanasiasa wa upinzani , lakini ameondoa uwezekano wa kukutana na rais Pervez Musharraf. Bhutto amerudia madai yake kuwa jenerali Musharraf ajiuzulu kama mkuu wa majeshi na kuondoa amri ya hali ya hatari , ambayo ameitangaza mwishoni mwa juma.Hapo mapema alijiunga na jaji mkuu aliyeondolewa madarakani Iftikar Chaudhry kutoa wito kwa raia kupinga dhidi ya amri hiyo ya hali ya hatari.

Katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na kundi la wanasheria, Chaudhry amesema kuwa serikali ya rais Musharraf haipashwi kuruhusiwa kuitengua katiba. Katika mji ulioko kusini magharibi ya nchi hiyo wa Multan , kiasi cha wanasheria 1,000 walipambana na polisi katika maandamano ambayo yanapinga amri hiyo ya hali ya hatari.Maandamano kama hayo pamoja na matukio ya kukamatwa watu wengine kadha, yametokea katika miji mingine kadha. Duru za upande wa upinzani zinasema kuwa kiasi cha wanasheria 3,500 , ambao waliongoza harakati za maandamano , wamo kizuizini.