1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD : Musharraf atangaza uchaguzi Februari

8 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C78u

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan amethibitisha kwamba uchaguzi mkuu wa bunge nchini Pakistan utafanyika kabla ya tarehe 15 mwezi wa Februari na ameahidi kujiuzulu wadhifa wake wa mkuu wa majeshi.

Shirika la habari la serikali nchini Pakistan limemkariri Musharraf akisema baada ya kuongoza mkutano wa Baraza la Usalama la taifa akisema kwamba mabaraza ya bunge la taifa na yale ya majimbo muda wake unamalizika katika tarehe tafauti na kwamba baada ya kuangalia hali hiyo imeamuliwa kufanya uchaguzi huo siku moja tarehe 15 mwezi wa Februari au kabla ya tarehe hiyo.

Televisheni ya taifa pia imeripoti kwamba Musharraf amerudia ahadi yake ya kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa majeshi kabla ya kula kiapo cha kipindi cha pili madarakani.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto amesema leo hii kwamba ahadi ya Rais Musharraf kufanya uchaguzi katikati ya mwezi wa Februari haitoshi na kuongeza kwamba lazima ajiuzulu ukuu wa majeshi ifikapo wiki ijayo.

Bhutto ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba lazima atangaze tarahe kamili ya uchaguzi,ratiba ya uchaguzi na tarehe hasa ya Musharraf kuachana na wadhifa wake wa kijeshi.

Bhuto ameahidi kuitisha maandamano makubwa hapo kesho mjini Rawalpindi na baadae kuandamana kutoka mji wa Lahore hadi Islamabad hapo Novemba 13 iwapo Musharraf hatotekeleza madai hayo na kubatilisha utawala wa hali ya hatari nchini humo.