1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad: Waislamu wenye siasa kali nchini Pakistan wakata vichwa vya mahabusu 13.

28 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7By

Waislamu wenye siasa kali huko Pakistan wamewakata vichwa mahabusu 13 waliowatuhumu kuwa ni majasusi wa serekali ya nchi hiyo. Kunyongwa watu hao yaonesha ni kulipizia kisasi mashambulio yaliofanywa na majeshi ya usalama dhidi ya ngome ya Shehe wa Kiislamu katika jimbo la kaskazini magharibi la nchi hiyo. Watu waliouliwa, wakiwemo wanajeshi sita na raia saba, walikamatwa na wapiganaji wa Kiislamu katika kizuwizi cha njiani karibu na mji wa Mingora. Wapiganaji hao wa Kiislamu wamepambana na majeshi ya usalama katika eneo hilo tangu ijumaa na inasemekana walikiteka kituo cha polisi katika kijiji cha jirani. Majeshi ya serekali yamepelekwa katika eneo hilo kuzuwia kujipenyeza wapiganaji wa Kiislamu kupitia mpaka na Afghanistan.

Inasemakan maelfu ya raia hivi sasa wanalikimbia eneo hilo la mapigano.

Na huko Afghanistan, majeshi yanayoongozwa na Marekani, yamewauwa wapiganaji wa Kiislamu 80 katika mji uliokuwa umeshikiliwa na Wataliban. Mapigano hayo katika mji wa Musa Qala katika jimbo la Helmand, eneo ambako bangi nyingi inapandwa, ni mapigano makubwa katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwezi wa Septemba. Hadi sasa wapiganaji zaidi ya 250 wameuliwa na hiyo inaonesha dalili kwamba majeshi ya Kimarekani na Kiengereza yanaanza kulidhibiti tena eneo hilo kutoka kwa Wataliban.