1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD: Wanajeshi wa Pakistan waendelea na operesheni ya kuwachakaza wanamgambo

11 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBjs

Milipuko mikubwa imesikika mapema leo katikati ya mji mkuu Islamabad huku wanajeshi wa Pakistan wakiendelea na operesheni yao ya kuwachakaza wanamgambo wa kiislamu ambao bado wamo ndani ya msikiti mwekundu wa Lal Majid.

Msemaji wa wizara ya ulinzi nchini Pakistan, Meja jenerali Wahid Arshad, amesema wanajeshi wanayasaska mahandaki yaliyojengwa chini ya msikiti huo ambamo wanamgambo wengi wamejificha na wanaendeleza upinzani mkali.

Maafisa wa wizara ya mambo ya ndani ya Pakistan wametangaza kuwa watu takriban 59 waliuwawa wakati wanajeshi wa serikali walipouvamia msikiti wa Lal Majid hivyo kumaliza mzozo wa msikiti huo uliodumu siku nane.

Kiongozi wa wanamgambo wa kiislamu ndani ya msikiti huo, Abdul Rashid Ghazi, ni miongoni mwa waliouwawa.

Huku wanajeshi wakiendelea kuwasaka wanamgambo waliosalia ndani ya msikiti huo, hofu inazidi kuhusu hatima ya mamia ya wanawake na watoto ambao walikuwa wakizuiliwa mateka.

Duru zinasema mamia ya mifuko ya kuhifadhia maiti imeagizwa hivyo kuongeza hali ya wasiwasi kwamba idadi ya waliouwawa kwenye uvamizi wa msikiti mwekundu huenda ikawa kubwa zaidi kuliko idadi iliyotolewa.