1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD:Bunge la Pakistan kuvunjwa kesho usiku

14 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CG1T

Bunge nchini Pakistan linapangwa kuvunjwa kesho usiku sawa na saa moja jioni za London, GMT ili kutoa fursa ya kujiandaa kwa uchaguzi ulitangazwa.kwa mujibu wa naibu Waziri wa habari Tariq Azeem bunge hilo litakuwa limekamilisha muhula wake wa miaka mitano.Serikali ya muda itaapishwa siku ya Ijumaa ili kujiandaa kwa uchaguzi wa Januari tarehe tisa kama ilivyotangazwa na Rais Pervez Musharraf wa Pakistan kufuatiwa hali ya hatari iliyoanza yapata majuma mawili yaliyopita.Waziri mkuu wa muda aidha anatarajiwa kutangazwa hapo kesho wakati bunge litakapovunjwa.Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22 kwa bunge kukamilisha muda na majukumu yake.Serikali za mikoa zinatarajiwa kuvunjwa tarehe 20 mwezi huu.

Wakati huohuo mwanasiasa wa upinzani na mcheza kriketi maarufu wa zamani Imran Khan anazuiliwa na polisi baada ya kutoka alikojificha.Mwanasiasa huyo alipanga kuhudhuria mkutano wa hadhara ili kupinga hali ya hatari iliyotangazwa,.

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto yuko katika harakati za kuungana na wanasiasa wengine wa Upinzani ili kupinga sheria ya Rais Musharraf,.Bi Bhutto anatoa wito wa kujiuzulu kwa kiongozi huyo aidha kutangaza kutoshirikiana na Rais Musharraf katika serikali moja.

Marekani iliyo mwandani wa Pakistan hasa katika vita dhidi ya ugaidi inapanga kumtuma Islamabad Naibu Waziri wa mambo ya kigeni John Negroponte.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanatoa wito kwa Marekani kumshinikiza Rais Musharaf.

''Sisi Amnesty International pamoja na mashirika mengine 11 makubwa ya kutetea haki za binadamu tunadai kuwa Pakistan isitishiwe misaada ya usalama zikiwemo huduma za kijeshi mpaka pale Rais Musharraf atakapobatili sheria ya hali ya hatari na kuwaachia wanasheria wakuu.''amesema T Kumar mkurugenzi wa Shirika la Amnesty International tawi la Asia na Pacific mjini Washington