1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD:jaji mkuu wa zamani ahimiza harakati za kurejesha demokrasia

6 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C79W

Jaji mkuu wa zamani nchini Pakistan Iftikhar Chaudhry amewatolea mwito raia kuunga mkono harakati za kutetea demokrasia nchini humo.

Chaudhry ametoa mwito huo alipokuwa anawahutubia mawakili kadhaa kwa njia ya simu.

Jaji huyo wa zamani amesema kuwa rais Pervez Musharraf amekiuka katiba ya Pakistan na kwamba umefika wakati sasa wa kujitolea kumpinga.

Wakati huo huo mamia ya mawakili wamepambana na polisi katika mji wa Multan polisi walitaka kuwazuia wasifanye maandamano. Maandamano hayo yalilenga kupinga amri ya hali ya hatari iliyotangazwa na rais Musharraf.

Taarifa zaidi zinafahamisha kuwa waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto yuko njiani kuelekea mji mkuu wa Islamabad amabako anatarajiwa kukutana na wanasiasa wengine wa upinzani ili kujadili mbinu za kukabiliana na hali iliyopo nchini Pakistan.

Rais George Bush wa Marekani kwa mara ya kwanza ametamka rasmi juu ya hali ya Pakistan na amemtaka mshirika wake jemadari Pervez Musharraf kurejesha demokrasia haraka na pia kuitisha uchaguzi pamoja na kuachia madaraka ya kijeshi.