1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD:Rais Musharraf na Benazir Bhutto kugawanya madaraka

29 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUg

Kiongozi wa Pakistan Rais Pervez Musharraf huenda akakubali kugawanya madaraka na Benazir Bhutto.Kulingana na waziri mmoja aliye mwandani wa Rais Musharraf masuala yote muhimu yameshajadiliwa na muafaka kuyahusu kufikiwa.Kwa mujibu wa mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini London anakoishi Bi Benazir Bhutto uhamishoni,Bwana Musharraf amekubali kuacha nafasi yake kama mkuu wa majeshi.Bi Bhutto anasubiri kujiuzulu kwa Rais Musharraf katika wadhifa huo ili aweze kurejea nyumbani kuwania nafasi ya Waziri mkuu .Benazir Bhutto anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Katika tukio jengine mahakama kuu nchini Pakistan isiyoegemea upande wa serikali inazidi kumshinikiza Rais Musharraf kwa kukubali kusikiliza kesi inayomtaka kujiuzulu kama kiongozi wa jeshi la taifa.

Rais Musharraf kwa upande wake aliye mwandani wa marekani na anayeunga mkono vita dhidi ya ugaidi anapanga kuwania tena wadhifa wa rais vilevile kiongozi wa jeshi ifikapo mwezi Septemba au Oktoba.Hata hivyo anashinikizwa kuondoka baada ya kuongoza utawala wa kijeshi kwa miaka 8.

Bi Benazir Bhutto alikuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke mwaka 88-90 na 93-96.Waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharrif aliyeondolewa katika mapinduzi mwaka 99 ametangaza kurudi Pakistan aidha kushiriki katika uchaguzi ujao mwanzoni mwa mwaka ujao.