1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD:Rais Mussharaf azidi kushinikizwa Nawaz Sharif kurudi nyumbani

24 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWR

Rais wa Pakistan Pervez Musharraf anakabiliwa na shinikizo za kisiasa huku waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif aliyemuondoa kwa mapinduzi akiahidi kurejea nchini mwake katika kipindi cha majuma kadhaa yajayo ili kushiriki katika uchaguzi wa rais.Mahakama kuu iliamua kuwa waziri mkuu huyo wa zamani aliyeshika wadhifa huo mara mbili mwaka 90-93 na 97-99 kabla kungolewa madarakani anaruhusiwa kurejea nchini mwake baada ya kuwa uhamishoni nchini Saudi Arabia na Uingereza.Kiongozi huyo wa zamani alielezea uamuzi huo kama ushindi dhidi ya utawala dhalimu.

Bwana Sharif aliyasema hayo akiwa mjini London.

''Nadhani tunahitaji kurejesha majeshi katika kambi zao.Nafikiri tunapaswa kulieleza waziwazi hilo.Sharti sheria idumishwe nchini Pakistan…katiba iheshimiwe …vilevile..mahakama isiegemee upande wowote…..na vyombo vya habari viwe huru.Hakuna njia nyengine yoyote kuhusu masuala haya''

Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika mapema mwaka ujao.Huu ni uchaguzi wa kwanza katika kipindi cha miaka mitano.Rais Musharraf anakabiliwa na shinikizo nchini mwake aidha jamii ya kimataifa kutoshiriki tena katika uchaguzi mkuu ujao kuwani urais na amri jeshi mkuu.Nchi yake aidha inazongwa na ghasia zinazosababishwa na wapiganaji wanaoaminika kuhusika na kundi la kigaidi la Al Qaeda.

Kwa mujibu wa msemaji wake Bwana Sharif hana nia ya kupatana na Rais Musharraf.Nawaz Sharif alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mashtaka ya kutaka kupindua serikali,kukwepa klulipa kodi na uhaini.Kulingana na serikali mashtaka hayo hayajafutwa.