1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel ilihusika na shambulio la Syria?

4 Februari 2013

Israel imeonyesha ishara kwamba ilifanya mashambulizi ya anga nchini Syria wiki iliyopita, huku Rais Bashar al-Assad akilituhumu taifa hilo la Kiyahudi kwa kujaribu kuidhoofisha nchi yake ambayo inakumbwa na vita.

https://p.dw.com/p/17XU3
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud BarakPicha: Reuters

Israel imeonyesha ishara japo sio wazi kwamba ilifanya mashambulizi ya anga nchini Syria juma lililopita, huku Rais Bashar al-Assad akilituhumu taifa hilo la Kiyahudi kwa kujaribu kulidhoofisha taifa lake hilo ambalo linakumbwa na vita.

Siku nne baada ya Syria kudai kuwa Israel inahusika na shambulio la anga katika kituo cha utafiti wa kijeshi karibu na mji mkuu wa Damascus, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak, amezungumza na waandishi wa habari mjini Munich, Ujerumani, lakini ameshindwa kuthibitisha kwamba Israel inahusika na shambulio hilo.

Barak jana aliwaambia wanadiplomasia wa ngazi za juu na maafisa wa masuala ya ulinzi katika mkutano wa usalama mjini Munich kwamba hicho kilikuwa ni kithibitisho kwamba wanaposema kitu huwa wanamaanisha. Israel haijathibitisha rasmi kuhusika na shambulio hilo, ingawa imekuwa ikizituhumu Iran na Syria kwa kulipatia silaha kundi la Hizbollah ambalo lilipambana na Israel katika vita vya mwezi mmoja mwaka 2006. Barak amesema hawadhani kama Syria inaruhusiwa kupeleka silaha za kisasa Lebanon.

Kiongozi wa Hizbollah, Hassan Nasrallah
Kiongozi wa Hizbollah, Hassan NasrallahPicha: picture-alliance/dpa

Syria yatishia kulipiza kisasi

Syria imetishia kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi hayo yaliyofanywa Jumatano iliyopita. Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan mkosoaji mkubwa wa Assad na Israel ameituhumu Israel kwa kuendeleza hali ya ugaidi ambapo amelaani shambulio hilo la anga akisema halikubaliki na linakiuka sheria za kimataifa na amekiita kitendo hicho ni uchokozi wa kigeni. Aidha, ameikosoa Iran kwa kuiunga mkono Syria.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi amesema amepokea kwa furaha uamuzi wa kiongozi wa muungano wa upinzani wa Syria Moaz al-Khatib kufanya mazungumzo na serikali ya Assad. Siku ya Jumamosi, Khatib alikutana na Salehi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, mjini Munich. Ama kwa upande wa mpango wake wa nyuklia, Salehi amesema Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu mpango huo, baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden kutoa ahadi ya kufanyika kwa mazungumzo hayo. Amesema wako tayari kuzungumza lakini lazima wahakikishe upande mwingine mara hii unkuja na nia halisi ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar SalehiPicha: Reuters

Ndani ya Syria kwenyewe watu wapatao 16 wameuawa miongoni mwao wakiwa watoto 10 na kamanda wa waasi, katika shambulio la kombora lililofanywa na jeshi la Syria kwenye mji wa Aleppo jana Jumapili. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la kusimamia haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza. Shirika hilo limesema kiasi watu 125 wameuawa jana Jumapili katika ghasia kuzunguka nchi nzima, miongoni mwao wakiwemo waasi 58.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail