1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Iran zashambuliana Mkutano wa Usalama wa Munich

Mohammed Khelef
18 Februari 2019

Mkutano wa Kimataifa juu ya Usalama uliofanyika mjini Munich, Kusini mwa Ujerumani, ulimalizika kwa majibizano makali kati ya Iran kwa upande mmoja na Marekani na Israel kwa upande mwengine.

https://p.dw.com/p/3DZPK
München MSC Javed Zarif
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Joensson

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, aliliambia jukwaa hilo la kimataifa kuhusu usalama ulimwenguni kwamba Israel na Marekani wanafanya matendo yanayovifanya vita vionekane jambo tukufu.

Akijibu tuhuma za nchi yake kujihusisha na mizozo kama ile ya Syria, Zarif alisema Iran iko Syria kwa kuwa ilialikwa rasmi za serikali ya Syria kwa lengo la kupambana na ugaidi, na si jenginelo, kinyume na mahasimu wao ambao amesema wanajiingiza Syria bila kualikwa na kwa maslahi ya kuwalinda magaidi:

"Tupo Syria kwa mualiko wa serikali ya Syria kwa lengo moja tu la kupambana na ugaidi, hakuna sababu nyengine yoyote ya kuwako huko. Nadhani mara ya mwisho nilipoangalia sheria za kimataifa, nilikuta kuwa kuingilia anga la Lebanon na kulitumia kuipiga Syria ni kuvunja sheria za kimataifa. Na jumuiya ya kimataifa, hata watu wa Ulaya wanaoamini juu ya sheria za kimataifa kuwa msingi wa usalama duniani wanatulaumu sisi na sio Waisraeli kwa kuvunja sheria za kimataifa." Alisema Zarif.

Uwezekano wa vita na Israel

Akiulizwa na mwandishi mmoja wa habari ikiwa alichokisema kinamaanisha kuwa kitisho cha vita na Israel ni kikubwa, Zarif alikiri kuwa ni kikubwa, lakini akiongeza kuwa ni kikubwa zaidi pale dunia ikiendelea kufumbia macho uvunjwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Benny Gantz Generalstabschef Israels
Benny Gantz, mkuu wa zamani wa jeshi la Israel na mgombea wa nafasi ya waziri mkuu kwenye uchaguzi wa Aprili 2019.Picha: AP

Hapo awali, Saudi Arabia - hasimu mwengine mkubwa wa Iran - ilikataa kuhudhuria mkutano huo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje, Adel bin Ahmed Al Jubeir kufuta ziara yake mjini Munich kwa kile kilichoelezewa kuwa ni sababu za kiratiba.

Hata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye hakuhudhuria na badala yake jawabu la nchi yake kwa hotuba ya Zarif lilitolewa na Benny Gantz, mkuu wa zamani wa jeshi la Israel na mpinzani mkuu wa Netanyahu kwenye uchaguzi wa Aprili, ambaye aliendeleza vitisho dhidi ya Iran.

"Chini yangu mimi, Iran haitaitisha Israel kwa kuzichukuwa Syria, Lebanon na Ukanda wa Gaza. Wala haitahujumu utawala makini kwenye Mashariki ya Kati. Chini yangu, Iran haitakuwa na silaha za nyuklia," alisema Gantz.

Siku ya mwisho ya mkutano huu wa Munich hapo jana, ilipangwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya Mashariki ya Kati, ambako daima kumekuwa na mzozo unaohusisha Marekani, Israel na Saudi Arabia kwa upande mmoja na Iran kwa upande mwengine.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/DW
Mhariri: Daniel Gakuba