1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kutokubaliana na uchunguzi wa kimataifa

7 Juni 2010

Israel imesema kuwa hatokubaliana na uchunguzi wa kimataifa dhidi ya hatua yake ya kuvamia na kuzuia meli iliyokuwa na misaada ya kiutu kwa ajili ya wapalestina wa Gaza.

https://p.dw.com/p/Njek
Maandamano dhidi ya Israel mjini Istanbul UturukiPicha: AP

Balozi wa Israel nchini Marekani Michael Oren, amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News cha Marekani, kuwa, nchi yake inawasiliana na Marekani kuangalia jinsi ambavyo uchunguzi huo utakavyofanyika.

Matamshi yake hayo yamekuja mnamo wakati ambapo Israel inawarejesha makwao, wanaharakati 19 wa Ireland waliyokuwa katika meli nyingine ya misaada ya kiutu kwa wapalestina iitwayo Rachel Corrie. Wanaharakati hao walikamatwa na majeshi ya Israel yaliyoivamia meli hiyo ilipokuwa ikijaribu kuingia Gaza ikiwa na shehena hiyo.

Jumatatu iliyopita, wanaharakati tisa waliuawa wakati makomando wa Israel walipoivamia meli yao ya kituruki iliyokuwa na misaada ya kiutu kwa ajili ya wapalestina wa Ukanda Gaza.

Kitendo hicho kilishutumiwa vikali na mataifa kadhaa ambapo wito ulitolewa wa kutaka kuondolewa kwa vizuizi dhidi ya Gaza. Uturuki ndiyo imekuwa mstari mbele kuikosoa Israel ambayo ni mshirika wake wa muda mrefu.Waziri Mkuu wa Uturuki, Recepp Tayyip Erdogan amesema vizuizi dhidi ya Ukanda wa Gaza ni lazima viondolewe na kuilaumu Israel kwa vitendo vya kigaidi.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/ZPR