1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Labour kujiunga na serikali ya Netanyahu ?

24 Machi 2009

Muwafaka umefikiwa kati ya Netanyahu na Barak:je,Labour itaidhinisha ?

https://p.dw.com/p/HISo
Benjamin NetanyahuPicha: AP

Taarifa kutoka Jeruselem, zinasema kwamba muwafaka umefikiwa kati ya waziri-mkuu-mteule wa Israel Benjamin Netanyahu wa chama cha LIKUD na waziri wa ulinzi wa Chama cha Labour Ehud Barak kuunda serikali ya muungano . Katika serikali hiyo,taarifa zasema Bw. Netanyahu , amejitolea kuheshimu mapatano ya mpito yaliotiwa saini na serikali iliopita.

Chama cha Labour kinachofuata siasa za mrengo wa shoto na kati hatahivyo, kinasemekana kugawika kuhusu kujiunga katika serikali itayoongozwa na Bw.Netanyahu mwnye msimamo mkali kuelekea wapalestina.Kikao maalumu cha Halmashauri-kuu ya chama cha Labour kimeitishwa alaasiri ya leo Kuzungumzia maafikiano yaliofikiwa mapema asubuhi ya leo kati ya Bw.Netanyahu na Barak.

Waziri-mkuu mteule Benjamin Netanyahu na Kiongozi wa chama cha Labour Ehud Barak, wametia saini mapatano yasio rasmi kufuatia majadiliano ya masaa 24 yalioanza jana. Alaasiri ya leo, Halmashauri Kuu ya Chama cha Labour yenye wajumbe 1,470, itakutana mjini Tel Aviv na jioni kabisa inatazamiwa kupiga kura ili kuamua iwapo chama cha Labour kijiunge na serikali mpya au la.

Katika maafikiano hayo,Benjamin Netanyahu ameriridhia kuheshimu mapatano yote ya kimataifa iliofunga Israel -tafsiri kuwa Netanyahu, ataheshimu mapatano ya muda iliofunga Israel na wapalestina. Isitoshe, kwa muujibu wa maafikiano ya mapema asubuhi ya leo, Bw.Ehud Barak,kiongozi wa Labour, atasalia katika wadhifa wake wa waziri wa ulinzi .

Kuna wabunge kadhaa wa chama cha Labour waliokasirishwa na hatua ya Bw.Barak ya kujiamulia pekee kujadiliana na LIKUD licha ya upinzani wao kujiunga na serikali ya Netanyahu. Mbunge wa KNESET Shelly Yechmovic, amesema kuwa,kujiunga na serikali ya Bw.Netanyahu ni sawa na "kifo cha uadilifu" kwa chama cha Labour.

Netanyahu alijitahidi sana kukishawishi chama cha Labour kujiunga na serikali yake ya mrengo wa kulia kwavile, hakupenda kuunda serikali yenye wingi mdogo ikiegemea tu kura za vyama vidogo vyenye siasa au itikadi kali za kidini .

Netanyahu alikwisha afikiana na vyama vya aina hiyo -kile cha uzalendo wa kiyahudi "Yisrael Beitenu" na kile cha itikadi kali ya dini ya kliyahudi "Shas party." Hatahivyo, waziri-mkuu mteule akihofia kuegemea sana vyama hivyo ili asije akagongana kisera na utawala wa rais Barack Obama wa Marekani alievinjari kusukuma mbele utaratibu wa amani kati ya Israel na Wapalestina.

kuunda serikali, Bw.Netanyahu atakuwa na jumla ya viti 66 katika Kneset-bunge lenye jumla ya viti 120.Hapo kabla, Netanyahu alishindwa kumshawishi waziri wa nje Bibi Tzipi Livni na chama chake cha KADIMA kujiunga na serikali yake.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Aboubakary Liongo