1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Chama cha Hamas zitasitisha mapigano huko Gaza

Othman, Miraji18 Juni 2008

Kuanzia kesho, Israel na Hamas zitaacha kupigana huko Gaza

https://p.dw.com/p/EMCT
Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert(kushoto), na waziri wa ulinzi, Ehud BarakPicha: AP

Israel imechukuwa wakati wa kutafakari juu ya uamuzi na njia mbali mbali zilioko mbele yake. Lakini sasa ni wazi kwamba serekali ya Israel imekubali kusitisha mapigano baina yake na Chama cha Wapalastina cha Hamas. Amri hiyo itaanza kufanya kazi kesho, alhamisi, saa 12 za asubuhi, kwa saa za Afrika Mashariki, na itadumu kwa miezi sita. Sasa amri hiyo itabidi itekelezwe na pande zote mbili.


Habari hiyo ilitangazwa na Redio ya Israel leo asubuhi, ikitajwa pia kwamba Israel itaanza kuitekeleza amri hiyo kutoka wakati huo uliotajwa. Pia ilitajwa kwamba waziri mkuu, Ehud Olmert, pamoja na waziri wa ulinzi, Ehud Barak, wametoa vibali vyao juu ya jambo hilo. Serekali ya Israel ilingoja kwanza arejee kutoka Misri mwakilishi wao waliompeleka huko kupata maelezo zaidi juu ya mapatano hayo na Chama cha Hamas. Misri ilikuwa mshenga katika jambo hilo. Jana waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud barak, alitangaza kwamba ni mapema kuzungumzia juu ya amri ya kusitisha mapigano.


"Uwezekano wa kufikia hali ya utulivu hivi sasa unachunguzwa. Bado ni mapema mno kutangaza juu ya utulivu huo, na ni sio wazi lini utaanza kufanya kazi na kwa muda gani. jambo hilo lazima lizingatiwe. Jeshi limejitayarisha kwa mambo yote, lakini ni muhimu kuitumia nafasi ya kuleta hali ya utulivu katika vijiji vinavouzunguka ukanda wa Gaza."


Kiongozi wa Chama cha Hamas, Khaled Meschaal, alisema huko Damascuss kwamba pindi Israel itakwenda kinyume na amri hiyo ya kusitisha mapigano, basi chama chake cha Hamas kitajibu pigo lolote. Hapo kabla maelezo juu ya amri hiyo ya kusitisha mapigano yalijulikana, na mara zikasikika sauti za kuitilia wasiwasi hali hiyo. Kwa mujibu wa makisio ya gazeti la kila siku la Israel, HAARETZ, masharti yaliowekewa amri hiyo ya kusitisha mapigano hasa yanaimarisha msimamo wa Chama cha Hamas katika mashauriano yake na chama hasimu cha Fatah. Israel, kutokana na masharti ya amri hiyo ya kuacha kushambuliana na Chama cha Hamas huko Gaza, inapoteza ushawishi wowote iliokuwa nao katika kivuko cha mpakani cha Rafah baina ya Misri na Ukanda wa Gaza. Na suala la kuachiliwa huru mwanajeshi wa Israel aliyetekwa nyara na wapiganaji wa Hamas, Gilad Schalit, bado linabakia sio hakika. Jambo hilo lilitangazwa na kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, Mahmud Zahar..


"Suala hilo halifungamani kabisa na mashauriano ya sasa. Hakuna mafungamano baina ya amri ya kusitisha mapigano na Schalit."


Suala la kuachiliwa huru mwanajeshi huyo wa Israel litazungumziwa mnamo wiki chache kutoka sasa. Pindi amri hiyo ya kusitisha mapigano itaanza kufanya kazi kesho na itabakia kwa siku tatu, Israel itafungua vivuko viwili vya mipakani na kuwachia kupita bidhaa kwendea Ukanda wa Gaza. Lakini hiyo haitamaanisha kuondosha kabisa kuuzi ngira ukanda huo, jambo ambalo sasa limedumu kwa mwaka mzima. Jana maroketi ya aina ya Kassam yalifyetuliwa kuelekea mji wa Israel wa Sderot kutokea Gaza. Inasemekana mtoto mmoja alijeruhiwa. Mji huo wa Sderot umeshambuliwa sana na maroketi ya Wapalastina na wakaazi wa mji huo wanaiona amri hiyo ya kusitisha mapigano kwa jicho la ati ati. Mkaazi mmoja wa mji huo alisema anaiona amri hiyo kuwa ni ujanja, na kwamba itawapa nafasi wapiganaji katika Gaza wajikusanyie silaha, na kwamba amri hiyo ni ya kulegalega mno kwamba dakika yeyote inaweza kuvunjwa. Na huko Gaza wakaazi wengi hawafikiri kwamba Israel itaitekeleza amri hiyo na kukomesha operesh-eni zake za kijeshi.


Marekani haijasema chochote juu ya amri hiyo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo alisema wao hawajuwi kama kweli kuna maafikiano hayo.