1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Hamas zafikia suluhu

Mohamed Dahman19 Juni 2008

Usitishaji wa mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas ambao umeanza kutekelezwa leo hii yumkini ukaleta utulivu wa muda Gaza lakini pia unaweza kusababisha madhara ya muda mrefu kati ya mahasimu hao wakubwa wawili.

https://p.dw.com/p/EN3D
Waziri Mkuu Ehud Olmert wa Israel kushoto akiwa na Waziri wake wa ulinzi Ehud Barak.Picha: AP

Pande zote mbili hazina uhakika suluhu hiyo inaweza kudumu kwa muda gani katika makubaliano hayo ambayo hayakuwahi kutokea katika siasa za kimataifa.

Israel bado inaliona kundi la Hamas kuwa la kigaidi wakati Hamas inaliona taifa la Israel kuwa ni taifa hasimu.

Makubaliano hayo yaliofikiwa chini ya usuluhishi wa Misri ambayo yameanza kazi leo alfajiri yamepokewa kwa mashaka na pande zote mbili.

Waisrael wengi wana hofu kwamba Hamas watutumia kipindi hicho cha utulivu kujilimbikizia silaha wakati Wapalestina wana wasi wasi kwamba usitishaji huo wa mapigano utaiwezesha Israel kuweka nadhari yake katika kuimarisha harakati zake za ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi.

Muda mfupi tu kabla ya kuanza kutekelezwa kwa usitishaji huo wa mapigano kombora la Israel limemuuwa mpiganaji mmoja wa Kipalestina na kumjeruhi mwengine katika eneo la uzio wa mpakani na Israel katikati ya Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema makubaliano ya usitishaji wa mapigano kati ya Israel na Hamas yanastahiki kujaribiwa lakini hajuwi yanaweza kudumu kwa muda gani.

Barak amesema uwezekano wa kufikia hali ya utulivu unachunguzwa na ni mapema mno kupiga upatu kwamba hali hiyo imefikiwa hasa na hata kama utapatikana haijulikani utadumu kwa muda gani. Amesema jeshi linajiandaa kwa chochote kitakachotokea na cha muhimu ni kutumia fursa iliyojitokeza kuleta utulivu katika eneo lote linalozunguka Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amelionya kundi la Hamas leo hii kwamba makubaliano hayo ni nafasi ya mwisho kwa kundi hilo la wanamgambo kuepusha kujiingiza kijeshi kwa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Katika mahojiano na gazeti la moja la Australia Olmert amesema wamefikia kikomo cha subira.

Amesema tokea Israel kujitowa Gaza miaka mitatu iliopita Waisrael 250,000 wanaoishi katika eneo linalozunguka Gaza imebidi wavumilie mashambulizi ya maroketi ya takriban kila siku kutoka kwa wanamgambo wa Kipalestina na kuongeza kusema kwamba hakuna nchi ingeliweza kuvumilia hali hiyo.

Mark Negev msemaji wa serikali ya Israel anasema wakati akitaraji kukomeshwa kwa mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza dhidi ya Israel na kujiimarisha kijeshi kwa kundi la Hamas huko Gaza pia ametaka kuona hatua zikichukuliwa kwa ajili ya kuachiliwa huru kwa Gilad Schalit mwanajeshi wa Israel anayeshikiliwa mateka huko Gaza jambo ambalo kiongozi wa kundi la Hamas huko Gaza Mahmud al Zahar anasema ni vitu visivyohusiana kwamba hakuna uwiano wowote wa kuweka chini silaha na suala la Schalit.

Pamoja na kuzuwiya mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ambayo inatawaliwa na kundi la Hamas makubaliano hayo yanaitaka Israel kuregeza vikwazo vyake dhidi ya Gaza ambapo takriban wakaazi wake milioni 1 nukta tano wanaishi kwa kutegemea misaada.