1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kuufunga mpaka wake wa kuingilia ukanda wa Gaza.

Halima Nyanza24 Desemba 2008

Wakati Mahujaji leo wakikusanyika katika mji mtakatifu wa Bethlehem, kusali katika mkesha wa Krismas, siku aliyozaliwa Yesu Kristo, Israel inaendelea kuufunga mpaka wake wa kuingilia eneo la Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/GMPl
Wakazi wa eneo la Ukanda wa Gaza katika Mamlaka ya Palestina, ambalo limekubwa na vurugu.Picha: AP

Israel imefuta uamuzi wake uliotoa mapema wa kufungua mipaka kuingia eneo la Gaza ,kwa ajili ya kuweza kupitishwa misaada muhimu ya kibinadamu, kufuatia mashambuklio mapya ya roketi yaliyofanywa katika ardhi ya nchi hiyo kutokea ukanda wa Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Israel Peter Lerner amesema msafara wa magari yaliyobena chakula na madawa kutoka ktika Mashirika ya Kimataifa yasiyo ya Kiserikali, ambayo yalipangiwa kuanza kuingia Gaza leo kupitia Israel, hayataruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Msemaji wa Jeshi la Israel amesema wapiganaji wa Kipalestina walifurumusha maroketi 12 katika ardhi ya nchi hiyo, baada ya Jeshi la nchi hiyo kuwaua wapiganaji watatu wa Hamas, hali ambayo imeongeza hofu katiika eneo hilo la Palestina.

Katika taarifa yao wapiganaji wa Hamas wamesema hatua hiyo ya mashambulio dhidi ya Israel ni kulipiza kisasi cha kuuawa kwa watu wao.

Habari zinasema kuwa hali ya vurugua iliyoendelea jana katika ukanda wa Gaza, baada ya utulivu wa siku mbili kunaondoa uwezekano wa Israel na kundi hilo la Wapalestina kuanzisha upya mpango wa usimamishaji wa mapigano.

Leo Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni anatarajiwa kuelekea Cairo Misri kwa mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak juu ya uwezekano wa kuongeza muda wa makubaliano ya kusimamisha mapigano, ambapo makubaliano ya awali ya miezi sita ya kusimamisha mapigano yalikwisha siku ya Ijumaa.

Hali hiyo ya ghasia inatokea katika kipindi hiki, ambapo leo usiku mahujaji wanakusanyika katika mji mtakatifu wa Bethlehemu kufanya ibada, katika mkesha wa Krismas siku aliyozaliwa Yesu Kristo.

Mahujaji wa Kikristo kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo nchi za kiarabu hukusanyika katika mji Mtakatifu wa Bethlehem kwa kufanya ibada wakati wa mkesha wa Krismasi.