1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulio yake ya nguvu dhidi ya Gaza.

Halima Nyanza29 Desemba 2008

Israel leo imekuwa ikiendelea kufanya mashambulio ya nguvu ya anga katika Ukanda wa Gaza, katika kipindi cha siku tatu mfululizo, huku ikitangaza mpaka wake na Gaza kuwa ni eneo la kijeshi lililozingirwa.

https://p.dw.com/p/GOb6
Vikosi vya Israel, vikiwa katika mpaka wake kuingia Gaza, ikiwa tayari imetangaza eneo hilo kuwa ni la kijeshi lililozingirwa.Picha: AP

Tangazo hilo la Kufungwa kwa eneo hilo la mpakani, huenda pia kukaisaidia Israel kuimarisha mashambuilio yake ya ardhini wakati wowote, jeshi la nchi hiyo litakapoagizwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Israel, hatua hiyo inamaanisha kwamba raia wote, wakiwemo waandishi huenda hawataruhusiwa kuingia katika eneo hilo la ukubwa wa kati ya kilomita 2 hadi nne kutokea Gaza.

Mashambulio hayo yanayofanywa na Israel kwa sasa ambayo yanalenga Chama cha Hamas, yameelezwa kuua raia 51, kati ya zaidi ya watu 312 waliouawa mpaka sasa.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, Christopher Gunness amesema wanawake na watoto ni miongoni mwa raia hao wasio na hatia waliouawa.

Amesema kwa sasa wanatayarisha orodha ya raia waliouawa katika shambulio hilo.

Shambulio hilo lililofanywa na Israel katika maeneo ya Hamas kwenye ukanda wa Gaza mpaka sasa limesababisha watu zaidi ya 1,400 kujeruhiwa.

Wengi ya waliokumbwa na shambulio hilo ni wanachama wa Hamas, chama ambacho kinaongoza eneo hilo la Ukanda wa Gaza tangu Juni,2007.

Siku ya Jumamosi, Israel ilifanya mashambulio ya nguvu ya anga dhidi ya Hamas ikiwa ni kulipiza kisasi ya mashambulio ya roketi yanayofyatuliwa katika ardhi ya nchi hiyo, kutokea ukanda wa Gaza eneo ambalo lina idadi kubwa ya watu duniani.

Israel imeapa kuendelea na mashambulio hayo yake, ambayo yanadaiwa kulenga wapiganaji wa Kipalestina wanaofanya mashambulio katika ardhi ya Israel, kama anavyothibitisha Mark Regev, Msemaji wa Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert kwa kusema kuwa operesheni hii itaendelea, itaendelea mpaka pale watakapopata usalama katika eneo la kusini na hadi pale raia wa Israel hawatakabiliwa tena na vitisho vya mashambulio ya roketi zinazofyatuliwa na Hamas.

Hata hivyo kwa upande wa Palestina nao wamesisitiza kuendeleo na mashambulio wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina, mpaka pale ardhi yao itakaporudishwa.

Akieleza kuhusu mashambulio hayo yanayofanywa dhidi ya vituo vya Hamas, Msemaji wa Chama hicho, Fawzi Barhoum ameeleza kuwa chama chake kitalipiza kisasi dhidi ya mashambulio hayo.

Amesema wataendelea na upinzani wetu katika pande zote, kama ilivyokuwa hapo awali. Hiyo ni pamoja na mashambulio ya kujitolea mhanga.

Katika hatua nyingine kiongozi wa Ujumbe wa Palestina katika mazungumzo ya amani na Israel, yanayoungwa mkono na Marekani, Ahmed Qurie amesema mazungumzo hayo kwa sasa yamesimamishwa kufuatia mashambulio hayo dhidi ya Gaza.

Amesema hakuwezi kuwa na mazungumzo wakati mashambulizi dhidi yao yamekuwa yakiendelea.

Maandamano kulaani mashambulio hayo na miito mbalimbali imeshatolewa mpaka sasa kutaka kukomeshwa kwa mashjambulio hayo yanayofanywa na Israel, huku Hamas nao wakitakiwa kuacha kufyatua roketi katika ardhi ya Israe.

Tayari Braza la UIsalama la Umoja wa Mataifa limekaa kikao cha dharura kujadili suala hilo, huku Jumuia ya nchi za Kiarabu ikikaa Jumatano kujadili hali hiyo.