1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafurahishwa na hatua ya mabalozi kuondoka mkutanoni

Kalyango Siraj24 Aprili 2008

'Hali ya Gaza ni kama ya kambi za Nazi' Balozi wa Libya

https://p.dw.com/p/Do9e
Moja wa vikao vingi vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.Wajumbe wa mataifa ya kimagharibi waliondoka nje baada ya kukasirishwa na mtamshi ya mwenzao kutoka Libya aliesema kuwa hali ya Gaza inafanana na ile ya kambi za Nazi wakati wa vita vikuu vya pili duniani.Picha: UN Photo/Eric Kanalstein

Israel imesifu wanadiplomasia wa nchi za magharibi kwa hatua yao ya kutoka nje ya mkutano uliokuwa ujadilie mgogoro wa mafuta wa Gaza,kufuatia matamshi ya balozi wa Libya ya kuifanananisha hali ya sasa ya eneo la Gaza kama ile ya wakati wa kambi za wafungwa za wakati wa Unazi.

Wajumbe wa nchi za Ubeligiji,Uingereza,Costa Rica, Ufaransa na Marekani waliokuwa katika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walitoka nje ya kikao hicho.Sababu ilikuwa kupinga matamshi ya mwenzao kutoka Libya,Giadalla Ettalhi.

Mjumbe huyo alitoa maneno ambayo yaliifananisha hali hiyo kama ile iliokuwa katika kambi za wafungwa wakati wa Nazi katika vita vya pili vya dunai.

Wengi wa wahanga wa kambi hizo walikuwa wayahudi.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Israel, Arye Mekel,amenukuliwa kusema kuwa wanawasiwasi kutokana na kile kilichotokea katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,akiongeza kuwa baraza hilo,lilikuwa katika hali alioiita kuchukuliwa mateka,na mataifa aliosema ambayo hayawajiki na wakati uliopita yakiwa yamehusishwa na ugaidi.

Israel iliweka marufuku ya eneo hilo la Gaza kutopata mafuta ambalo linaloongozwa na kundi la Hamas,kama njia ya kuliadhibu.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa utalazimishwa kusitisha huduma za kimisaada ikiwa halitapata mafuta.Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Angela Kane amesema kuwa usambazaji wa chakula kwa watu wakimbizi 650,000 ,pamoja na ukusanywaji wa takataka kutoka kwa takriban watu 500,000 utasimamishwa mara moja.

Vikwazo vya Israel ili kulishurutisha kundi la Hamas kuachana na uvurumishaji wa maroketi katika ardhi yake ndio kumesababisha uhaba wa mafuta.

Lakini Israel inasema Hamas inakataa kimakusudi kusambaza mafuta hayo.Asili mia 80 ya raia wa Gaza hutegemea misaada ya kiutu ambapo chakula cha Umoja wa Mataifa kinawahudumia takriban watu milioni moja wengi wao wakiwa ni watoto.

Lakini Bi Kane ameonya kuwa msaada kama huo uko hatarini kutokana na masharti magumu kuhusu usambazaji wa mafuta,yaliyowekwa na Israel mapema mwezi huu baada ya wanamgambo wa Kipalestina kushambulia kituo cha mafuta cha Nahal Oz ambapo wanajeshi wawili wa Israel waliuawa.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa Israel haijatoa mafuta ya Petroli tangu Machi 18 na mafuta ya diesel tangu April 2.

Katika mantiki hiyo mjumbe wa Libya akaifananisha hali hiyo kama ile ya vita vikuu vya pili vya dunia katika kambi za Nazi.Baadhi ya wajumbe hawakufurahishwa na tamko hilo na wakaondoka mkutanoni.

Hatua ya wanadiplomasia hao kuondoka mkutano wakiongozwa na balozi wa Ufaransa,Jean-Maurice Ripert,ilisababisha kikao hicho kufikia mwisho papo hapo.Kilikuwa kinajadilia taarifa kuhusu hali ya Gaza.

Haya yote yametokea wakati kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas akiwa katika zaira rasmi nchini Marekani ambapo atakutana na rais Bush kujadilia njia za kuendeleza mazungumzo ya amani yaliyokwama.

Inasemekana kuwa Abbas anataka utawala wa Bush kuishinikiza Israel kuacha upanuzi wa makazi ya kiyahudi inayoendeleza katika ukanda wa magharibi wa mto Jordan,ambao anahisi ni muhimu kuweza kuyasukuma mbele mazungumzo hayo.