1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yalaumiwa na Baraza la Haki za Binadamu la UM

28 Septemba 2010

Israel yasema uchunguzi ni wa upande mmoja

https://p.dw.com/p/PORa
Wakereketwa wa kiisraeli wanaodai amani.Picha: AP

Israel, imelaumiwa mno na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi hapo jana ; na imetakiwa itake radhi kwa kuivamia marekebu iliokuwa ikipeleka shehena za misaada Mwambao wa Gaza.

Tuhuma hizo zinafuatia uchunguzi uliobaini kuwapo ushahidi unaotilia nguvu kufunguliwa Israel mashtaka kwa kisa kile kilichosababisha vifo. Israel ambayo si mwanachama wa Baraza hilo, imelituhumu kuelemea mno upande mmoja.

 "Wahalifu wote waliohusika na mkasa huu lazima wawajibishwe.Israel inapaswa kubebeshwa jukumu kwa haya yaliotokea."-mjumbe wa Palestina aliambia Baraza hilo la haki za binadamu la UM mjini Geneva jana.Akaongeza kudai kwamba, wahanga wanapaswa kulipwa fidia na Israel, inabidi kuomba radhi kwa wale wote walioteseka na vitendo vile.

Uchunguzi uliofanywa na Baraza la haki za Binadamu la UM juu ya kisa cha Mei 31, mwaka huu, ulisema wiki iliopita kuwa, kuna ushahidi dhahiri-shahiri unaowezesha Israel kufunguliwa mashtaka kwa mauaji na mateso pale wanajeshi wake walipoivamia meli ile na kupelekea wakereketwa 9 wa haki za binadamu wa kituruki kuuwawa.

Ripoti hiyo kali juu ya uchunguzi uliofanywa kuhusu mkasa ule, ulitupilia mbali hoja iliotoa Israel kuwa, wakereketwa waliokuwa wakipeleka shehena za misaada Gaza, walitumia nguvu na hivyo kuhalalisha uamuzi wa askari-jeshi wa Israel kufyatua risasi.

"Hakuna silaha za kushambulia zilizopakiwa ndani ya marekebu zile.."-alidai Karl Hudson-Philips,alieongoza uchunguzi uliofanywa juu ya kisa kile.

Aliliambia jana Baraza la Haki za binadamu kwamba, sita kati ya waliouwawa, walipoteza maisha kwa kufyatuliwa risasi moja kwa moja ,2 kati yao , walipigwa risasi baada ya kuwa wamejeruhiwa vibaya na hawakuweza hata kujikinga.

Uturuki,ambayo raia zake 9 ndio waliouwawa, imesema kuwa, uchunguzi umeweka hesabu juu ya kilichotendeka sawa.Tangu awali lakini, Israel, imeukataa kuukubali uchunguzi huo na kueleza ni "ulioelemea upande mmoja tu".

Balozi wa Israel , alikariri jana msimamo wa nchi yake na kueleza matokeo ya uchunguzi huo ni ya "upande mmoja na yaliovuka mpaka".

Kundi la nchi za kiislamu pamoja na washirika wake lliikosoa mno Israel mbele ya Baraza hilo mjini Geneva.Limeituhumu Israel kwa kuonesha ukatili na maguvu yasiojali huko Mashariki ya Kati.

Marekani nayo kwa upande wake leo, imeukosoa uchunguzi juu ya uvamizi wa Israel wa marekebu zilizokuwa zikielekea Gaza.Marekani, imelitaka Baraza hilo la Haki za Binadamu la UM kuizuwia ripoti hiyo kutumika kuchafua mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE/AFPEUhariri:Abdul-Rahman