1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaongeza muda wa kusitisha mapigano Gaza, Hamas yakataa masharti

27 Julai 2014

Israel imerefusha hatua ya kusitisha mapigano kwa sababu za kiutu ukanda wa Gaza kwa saa 24, lakini Hamas , imesema itakubali kusitisha mapigano iwapo majeshi ya Israel yataondoka katika ardhi ya Gaza.

https://p.dw.com/p/1CjSl
Israel Gazastreifen Nahost-Konflikt
Mizinga ya vifaru vya Israel imesita kwa sasa kushambulia GazaPicha: REUTERS

Mawaziri wa Israel wametoa ishara kuwa matumaini ya makubaliano ya kweli ya kumaliza mzozo huo uliodumu kwa muda wa siku 20 sasa na Hamas na washirika wake, ambapo kiasi ya wakaazi wa Gaza 1,050, wengi wao wakiwa raia , wameuwawa, na wanajeshi 42 wa Israel pamoja na raia watatu wameuwawa , ni madogo.

"Kwa ombi la Umoja wa Mataifa, baraza la mawaziri la Israel limeidhinisha hatua ya kiutu ya kusitisha mapigano hadi usiku wa manane Jumapili," afisa, ambaye hakutajwa amesema katika taarifa baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika mjini Tel Aviv kumalizika. "Jeshi la Israel litachukua hatua dhidi ya aina yoyote ya ukiukaji wa hatua ya usitishaji wa mapigano."

Israel / Gazastreifen / Soldaten
Wanajeshi wa Israel katika doriaPicha: Reuters

Wakaazi wa Gaza watafuta miili ya wahanga

Jana Jumamosi , wakaazi wa Gaza walichukua fursa ya kusitishwa mapigano kuwatafuta watu waliouwawa na kuhifadhi chakula, wakimiminika mitaani baada ya kuanza kwa hatua hiyo ya kusitisha mapigano na kugundua uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo.

Misimamo ya Israel na Hamas kuhusiana na kusitisha uhasama kwa muda mrefu imeendelea kubakia mbali.

Hamas inataka kusitishwa kwa hatua ya Israel na Misri ya kulizingira eneo la Gaza kabla ya kukubaliana kuhusu kusitisha uhasama. Maafisa wa Israel wamesema makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano ni lazima yaruhusu jeshi kuendelea na kusaka mahandaki na njia za chini ya ardhi za Hamas ambazo zinavuka mpaka wa Gaza.

Waffenruhe bringt Zerstörung im Gazastreifen zum Vorschein 26.07.2014
Baada ya kusitishwa mapigano , uharibifu katika GazaPicha: imago

Israel inasema baadhi ya njia hizo za panya zinafika ndani ya ardhi ya Israel na zina lengo la kufanya mashambulizi dhidi ya raia wao. Njia nyingine za chini ya ardhi zinatumika kupitishia silaha na nyingine kama maeneo ya Hamas ya kuhifadhia silaha.

Jeshi la Israel IDF, limesema limegundua mashimo manne ya aina hiyo ndani ya Gaza wakati wa kipindi cha kusitisha mapigano jana Jumamosi.

Maafisa wa Israel wameongeza kuwa vikosi vyake vitaendelea kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wa hatua ya kusitisha mapigano, na kuongeza kuwa jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua dhidi ya njia hizo za chini ya ardhi katika kipindi hicho chote cha saa 24.

Paris Außenministertreffen Gaza Konflikt Gruppenfoto
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya magharibi katika mkutano wao mjini ParisPicha: picture-alliance/dpa

Amesema kuwa baraza la mawaziri litakaa kikao tena leo Jumapili (27.07.2014) kutafakari kuendelea na operesheni hiyo "hadi utulivu utakaporejea kwa raia wa Israel kwa kipindi kirefu."

Hali ya wasi wasi yaongezeka

Mzozo wa Gaza umeongeza hali ya wasi wasi miongoni mwa Wapalestina katika eneo la Jerusalem ya mashariki ambalo hukaliwa na Waarabu pamoja na ukingo wa magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.

Wauguzi wamesema Wapalestina wanane wameuwawa siku ya Ijumaa katika tukio karibu na mji wa Nablus na Hebron katika Ukingo wa Magharibi , vifo ambavyo vinafanana na vuguvugu la maandamano dhidi ya utawala unaoendelea wa Israel katika eneo hilo.

Notärzte in Gaza Arbeit in Lebensgefahr
Gari ya kubeba wagonjwa mjini GazaPicha: DW/S. al Farra

Katika upande wa diplomasia , juhudi za kimataifa kuleta hatua ya kusitisha uhasama na kupatikana kwa makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano yanaongozwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry mjini Paris.

Kerry ambaye amekuwa akiongoza juhudi za kimataifa kumaliza mapigano hayo, aliwasili mjini Paris jana Jumamosi ambapo alikutana na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Italia, Uingereza, Ujerumani , Uturuki na Qatar.

"Sisi sote tunatoa wito kwa pande zinazohusika kurefusha hatua hiyo ya kiutu ya kusitisha mapigano ambayo iko kwa sasa," Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amesema baada ya mkutano huo.

Hali ya kiutu katika eneo la Gaza hata hivyo inabaki kuwa mbaya , ambapo maji na madawa yakikosekana na kufikia katika hali ya hatari. Umeme pia unakosekana kutokana na kuharibiwa katika mapigano.

Israel Gazastreifen Nahost-Konflikt
Mama wa Kipalestina akiangalia uharibifu wa eneo lakePicha: REUTERS

Hospitali kadhaa zimeshambuliwa na majeshi ya Israel pamoja na makombora katika siku za hivi karibuni, na kusababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo. Jeshi la Israel linadai kuwa Hamas na makundi mengine ya wanamgambo yanaendesha shughuli zao karibu na vituo hivyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae

Mhariri: Caro Robi