1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yataka mpango wa amani wa Wasaudi uvuvuliwe.

22 Oktoba 2008
https://p.dw.com/p/Fewt
Rais wa Israel Shimon Peres.Picha: AP

Wapalestina wameelezea matumaini yao kwamba wito wa Israel kutaka mpango wa amani uliowahi kupendekezwa na Saudi arabia ufufuliwe upya, unaweza kusaidia kupatikana hatua ya maendeleo katika juhudi za kidiplomasia ambazo zimekwama kwa miaka kadhaa sasa. Wito huo wa Israel ulitolewa awali na Rais Wa Israel Shimon Peres alipomtaka Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia kuupa msukumo mpango huo ulioidhinishwa miaka sita iliopita.

Mpango huo unaojulikana kama "ardhi kwa ajili ya amani "unazungumzia utayarifu wa Dola za kiarabu kuitambua kikamilifu Israel ikiwa itazirudisha ardhi zote zinazokaliwa, ilizoziteka katika vita vya siku sita 1967 na kupatikana pia suluhisho la haki la wakimbizi wa kipalestina.Misri na Jordan ni nchi pekee za kiarabu ambazo hadi sasa zimesaini mkataba kamili wa amani na Israel.

Rais wa Israel Peres alisema mpango huo ni juhudi nzuri na zinazoweza kuleta faraja, na ni msingi wa majadiliano ya kimataifa baina ya Israel na nchi za Kiarabu. Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak naye pia amezungumza kwa lugha sawa na hiyo. Kiongozi wa ujumbe wa wapalestina katika mazungumzo na Israel Ahmed Qurei akasema a anafikiri Bw Barak na Kiongozi wa Kadima , waziri wa mambo ya nchi za nje Bibi Tzipi Livni wanakubaliana kuhusu hilo. Bibi Livni yumo katika jitihada za kuunda serikali ya mseto na vyama vyengine na kuchukua jukumu la Waziri mkuu , baada ya kujiuzulu Be Ehud Olmert kutokana na kashfa ya rushwa .

Qurei alisema Bibi Livni ambaye ni waziri mkuu mteule amekua ni mwenzake katika duru nyingi za mashauriano ya amani kati aya Israel na wapalestina.

Jana Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saudi arabia, Saud al-faisal alisema anatumai Bibi Livni atafuata muongozo wa Rais Peres wakati atakapounda serikali na kuanza kufanya kazi kama Waziri mkuu.

Livni ameashiria kuwa ataendelea na mazungumzo ya amani na rais Mahmoud Abbas chini ya uungaji mkono wa Marekani ambayo yalianzishwa mwaka mmoja uliopita na waziri mkuuOlmert anayeacha madaraka.

Mabishano juu ya makaazi ya wayahudi katika ukingo wa magharibi na tafauti miongoni mwa wapalestina ni miongoni mwa mambo makuu yaliovuruga matumaini ya Marekani kujaribu kuzishawishi pande hizo mbili kufikia makubaliano ya a amani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.