Maadhimisho ya Israel
8 Mei 2008
Isreal inaadhimisha mwaka wa 60 tokea kuundwa baada ya kupitia mitihani mizito katika historia yake.
Lakini imeweza kuhimili mitihani hiyo.
Waisraeli wanaadhimisha mwaka wa 60 wa nchi yao kwa sherehe mbalimbali ikiwa pamoja na hotuba za viongozi kuwapongeza na kuwakumbuka waasisi wa wa nchi hiyo.Sherehe zilianza kwa kupandisha bendera kwenye mlima wa Herzl uliopo Jerusalem.Majeshi ya usalama yalikuwa katika hali ya tahadhari kutokana na wasiwasi mashambulio ya wapiganaji wa kipalestina.
Wakati Israel inaadhimisha miaka 60 tokea kuundwa, wapalestina wanajitayarisha kuadhimisha miaka 60 ya wanachoita "Nakba" maafa.
Israel imejengwa na watu wa taifa jipya na la zamani baada ya kukumbwa na maafa makubwa barani Ulaya.
Utawala wa mafashisti nchini Ujerumani ulianzisha kampeni ya kuwaangamiza wayahudi milioni sita barani Ulaya.
Na hata baada ya Israel kuundwa nchi hiyo imepitia mitihani mizito kutokana na uhasama na jirani zake- nchi za kiarabu.
Lakini nchi hiyo imeweza kuhimili mitihani hiyo mizito. Kwani tokea kuundwa kwake miaka 60 iliyopita waisraeli wameshapigana vita mara kadhaa na jirani zao.
Maalfu ya waisrael mjini Jerusalem wanashiriki katika maadhimisho ya nchi yao wakati ambapo mustakabal wa kisiasa wa waziri mkuu wa nchi hiyo bwana Ehud Olmert umo mashakani kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Akiwapongeza waisraeli katika madhimisho ya taifa lao rais wa Ujerumani Horst Köhler amesisitiza kuwa kuendelea kuwapo kwa taifa la Israel ni nyanja ya msingi katika sera ya nje ya Ujerumani. Rais Köhler amesema Ujerumani wakati wote itasimama kutetea haki ya waisraeli ya kuishi maisha ya amani. Lakini pia ameeleza kuwa msingi wa amani ya kudumu katika mashariki ya kati ni kukomeshwa umwagikaji damu.