1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia njiani kuunda serikali mpya ama uchaguzi wa mapema

Mohammed Khelef
21 Agosti 2019

Rais Sergio Manttarella wa Italia ameanza mazungumzo na vyama vya siasa kuutatua mkwamo wa kisiasa kwa ama kuundwa kwa serikali ya 67 tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia au kufanyika uchaguzi wa mapema

https://p.dw.com/p/3OGFM
Giuseppe Conte
Picha: Reuters/C. de Luca

Hatua hii ya Rais Manttarella inafuatia uamuzi wa siku ya Jumanne (Agosti 20), ambapo Waziri Mkuu Giuseppe Conte alilitangazia bunge kwamba anaondoka kwenye wadhifa huo, baada ya kumshambulia vikali waziri wake wa mambo ya ndani, Matteo Salvini, akimtuhumu kwa kuizamisha serikali ya mseto na kuhatarisha uchumi wa taifa hilo la kusini mwa Ulaya kwa maslahi binafsi na ya kisiasa.

"Kuitisha uchaguzi ni msingi wa demokrasia, lakini kuitisha kuandaa uchaguzi kila mwaka ni kutokuwajibika. Uamuzi wa waziri wa mambo ya ndani katika wiki za hivi karibuni unadhihirisha ukosefu wa kuwajibika kitaasisi na upuuzaji mkubwa wa utamaduni wa kikatiba," alisema Conte.

Kauli hiyo nzito ya Waziri Mkuu Conte dhidi ya Salvini ilikuwa inarejea uamuzi wa tarehe 8 mwezi huu wa Agosti, ambapo kiongozi huyo wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, League, alitangaza kwamba ushirikiano wake na Vuguvugu la Nyota Tano linaloongozwa na Conte ulikuwa umekufa na akataka uitishwe uchaguzi mpya. 

Akishangiriwa na wenzake bungeni, Salvini alisema aliamua kujitoa kwenye serikali na Conte kwa kuwa muungano wao ulikuwa umeshindwa kuafikiana katika kila hatua ya uamuzi na utekelezaji, kuanzia kwenye kamati, bungeni na hata kwenye baraza la mawaziri, huku akidai kwamba jukumu lake kama waziri wa mambo ya ndani lilikuwa ni "kuifanya Italia iwe salama."

Hasira za Salvini kuelekea Umoja wa Ulaya

Regierungskrise in Italien | Matteo Salvini
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini.Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Salvini alimkosoa Conte kwa kuegemea sana kuwaridhisha wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels badala ya kuwatumikia wapigakura wa Italia.

"Wao wanaitaka nchi ya pili kwa uchumi mkubwa wa viwanda barani Ulaya kuheshimu kanuni za ovyo, wakati kwa miaka kadhaa Ufaransa na Ujerumani hazijali kanuni ambazo wao wanataka kuzitumia kuharibu maisha ya wanawake na wanaume huru milioni 60 wa Italia," alisema Salvini.

Awali ilikuwa ni Salvini aliyekuwa akiahidi mara kwa mara kuwa serikali hii iliyodumu kwa miezi 14 ingelikaa hadi miaka mitano iishee, lakini kwa sasa anaonekana kutaka kutumia uungwaji mkono wa wapigakura kuingia uchaguzini ili awe waziri mkuu wa Italia.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema huenda bahati nasibu hii ya kisiasa iikamgeukia mwenyewe Salvini, kwani tayari wawakilishi wa Vuguvugu la Nyota Tano na wale wa chama cha mrengo wa kati cha Democrat wanajadiliana uwezekano wa kuunda serikali mpya ya mseto na kukiweka chama cha League kuwa cha upinzani, huku ukiifanya Italia kuongozwa na serikali inayoelekea zaidi siasa za wastani. 

Rais Mattarella alitazamiwa kukutana na kila chama kuanzia saa 8:00 mchana wa Jumatano (Agosti 21) na kuendelea na vikao hadi Alhamisi saa 9:00 mchana, kuangalia uwezekano wa kuundwa kwa serikali nyengine ya mseto ama kuitisha uchaguzi mpya ikiwa ni miaka mitatu na nusu kabla ya muda.

Reuters/dpa