1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa ugaidi anayetengeza vitambulisho bandia akamatwa

Caro Robi27 Machi 2016

Polisi nchini Italia wamemkamata mwanamume mmoja raia wa Algeria anayeshukiwa kutengeneza vitambulisho bandia vilivyotumiwa na washukiwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Paris na Brussels.

https://p.dw.com/p/1IKOB
Picha: picture alliance/dpa/M. Bazzi

Kikosi cha polisi wa kupambana dhidi ya ugaidi nchini Italia kimemkamata Djamala Eddine Ouali mwenye umri wa miaka 40 katika mji mdogo ulioko kusini mwa Italia. Ripoti zinaarifu kuwa mshukiwa huyo alikuwa akisakwa na vikosi vya usalama baada ya waranti wa kimataifa kutolewa dhidi yake.

Ouali anatuhumiwa kwa kutengeneza vitambulisho na hati bandia zilizotumika na wahamiaji haramu na washukiwa wa ugaidi.

Huku hayo yakijiri, waendesha mashitaka wa Ubelgiji wamemfungulia mashitaka ya mauaji ya ugaidi na kujihusisha na kundi la kigaidi, mshukiwa anayeaminika alikuwa mshambuliaji wa tatu wa mashambulizi ya Brussels yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wiki iliyopita.

Mshukiwa huyo aliyekamatwa Alhamisi usiku ametambulia kwa jina Faycal C. Wachunguzi wa mashambulizi ya Brussels wanaamini ndiye mshambuliaji wa tatu aliyenaswa na kamera katika uwanja wa ndege akiwa na washambuliaji wengine wawili waliojitoa muhanga.

Maandamano kuwakumbuka waathiriwa yafutiliwa mbali

Wakati huo huo, maandamano ya amani ambayo yalikuwa yafanyike leo Brussels kuwakumbuka waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Brussels yamefutiliwa mbali kwasababu za kiusalama.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga wa mashamulizi ya Brussels Ibrahim El Bakraoui
Mshambuliaji wa kujitoa muhanga wa mashamulizi ya Brussels Ibrahim El BakraouiPicha: Reuters/Haberturk newspaper

Kufutiliwa mbali kwa maandamano hayo kunadhihirisha changamoto za kiusalama na hali ya taharuki iliyopo katika nchi za Ulaya kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Serikali ya Ubelgiji inakabiliwa na shutuma kali kwa kuzembea katika kukabiliana na kitisho cha ugaidi. Mawaziri wa nchi hiyo wamesisitiza kuwa walifanya kila waliloliweza kuepusha mashambulizi ya Jumanne na kuufuatlia mtandao wa kigaidi nchini humo ambao unahusishwa na mashambulizi ya Paris.

Watu wengi nchini Ubelgiji na katika nchi nyingine za Ulaya wanaamini nchi hiyo ilishindwa kuchukua hatua madhubuti kupambana dhidi ya ugaidi na kuwazuia raia wake kwenda Syria kupigana na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Mawaziri wawili wa Ubelgiji walitaka kujiuzulu baada ya taarifa kuibuka kuwa mmoja wa washambuliaji Ibrahim El Bakraoui, raia wa Ubelgiji alikuwa amerejeshwa nchini humo kutoka Uturuki baada ya kutajwa na Uturuki kuwa ni mpiganaji wa kigaidi.

Usalama umeimarishwa katika miji mikuu ya nchi za Umoja wa Ulaya na hali ya tahadhari imetangazwa katika baadhi ya nchi hizo. Mtu mwingine aliyekamatwa Ubelgiji na kutambuliwa kwa jina Rabah N. pia alishitakiwa Jumamosi kwa kuhusika katika jaribio la kuishambulia Ufaransa.

Waathirwa 24 watambuliwa rasmi

Huku zoezi gumu la kuwatambua waathiriwa wa mashambulizi ya Brussels likiendelea, maafisa wamesema waathirwa 24 kati ya 31 ya waliouawa wametambuliwa rasmi. Kumi na moja kati ya waliotambuliwa ni raia wa kigeni.

Maafisa wakiutathmini uwanja wa ndege wa Zaventem ulioharibiwa katika shambulizi
Maafisa wakiutathmini uwanja wa ndege wa Zaventem ulioharibiwa katika shambuliziPicha: picture alliance/ZUMA Press/Geert Vanden Wijngaert

Kati ya watu 340 waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo mawili, 62 kati yao bado wako katika chumba cha kuwahudumia wagonjwa mahututi.

Na maafisa wa uwanja wa ndege wa Brussels wameanza kutathmini uharibifu wa uwanja wa ndege wa Zaventem uliolongwa katika mojawapo ya mashambulizi ya Jumanne.

Wahandisi waliruhusiwa kuchunguza majengo ya uwanja huo kung'amua iwapo yako imara na kutathmini iwapo ukarabati unaweza kufanywa haraka. Uwanja huo wa ndege huwahudumia zaidi ya wasafiri milioni 23.5 kwa mwaka. Maafisa wamesema huenda ukafunguliwa tena baada ya Jumanne wiki ijayo.

Takriban safari 600 za ndege za kila siku zitokazo kutoka uwanja huo wa Brussels, zimefutuliwa mbali au kuelekezwa kwingine tangu mashambulizi hayo ya Jumanne.

Kutatizika huko kwa usafiri kunawatia wasiwasi raia wa nchi za Ulaya ambao wanahofu kuwa huenda kuna majihadi ambao bado wanapanga kufanya mashambulizi zaidi ya kigaidi.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/ap

Mhariri: Isaac Gamba