1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ivory Coast kupambana na Italia.

9 Agosti 2010

Didier Drogba akosa kushiriki mpambano wa kirafiki kwasababu ya jeraha.

https://p.dw.com/p/Ofdn
Didier Drogba wa Ivory Coast kushoto,aking'ang'ania mpira katika mashindano ya kombe la dunia mwaka huu dhidi Korea kaskazini.Picha: AP

Imebainika bayana kuwa aliyekuwa kocha wa timu ya Marseille ya Ufaransa huenda akapewa kigongo cha uongozi wa Ivory Coast, huku mchuano wa kirafiki wa hapo kesho dhidi Italia katika uga wa Upton ukiwadia.

Baada ya Sven Goran Eriksson kuipungia Ivory Coast mkono wa Buriani kombe la dunia lilipomalizika, rais wa shirikisho la soka nchini humo, Jacques Anouma, amemdokezea Gili huenda akarithi mikoba ya kikosi hicho, ikizingatiwa kuwa ameshazifunza timu ya vijana ya taifa na timu kuu vilevile katika miaka mitano nyuma.

Kuhusu shika mshike hiyo ya hapo kesho kati yao na Italia, mchezaji nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba, hakutajwa kushiriki na wenziwe 26 hapo kesho kutokana na maumivu alio nayo  baada ya operesheni aliofanyiwa ya mshipa wa Hernia iliomsababisha pia kutoshiriki vilivyo hapo jana jumapili wakati timu yake Chelsea ilipotifuana na Manchester United na Manu ikaibuka mshindi wa mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu wa Community Shield kwa mabao 3-1

Ndugu wawili wapya bidhaa moto za hivi karibuni za timu ya Manchester City ,Yaya Toure na mwenziwe Kolo Toure, wanatarajiwa kushiriki mpambano wa hapo kesho pamoja na mfungaji wa Chelsea, Salomon Kalou, na mlinzi wa Arsenal, Emmanuel Eboue.

Mpambano huo pia unatarajiwa kumpa nafasi kocha mpya wa Italia, Cesare Prandeli, kuchagua kikosi kipya cha timu ya taifa.

Prandelli amechukua nafasi ya Marcello Lippi aliyesita kuwa kocha wa timu hiyo, baada ya kushindwa Italia mabao 3-2 na Slovakia katika kombe la dunia.

Tukielekea Ufaransa kwa michuano ya Ligue 1, ambapo timu ya Marseille, waliongoza msimu uliokwisha, inaonekana bahati haikuwaangukia safari hii ,maana ulikuwa ni mwanzo wenye aibu waliposhindwa kulitetea taji hilo baada ya kufungwa mabao 2-1 na Caen juzi Jumamosi usiku.

Kunako dakika tano za mwisho Youssef El arabi wa Caen  alipachika mkwaju wavuni mwa Marseille ulio unyamazisha umati uliokusanyika katika uwanja huo wa Velodrome.

Marseille wenyeji walionekana kulemewa katika mechi nzima, lakini walibahatika kwa bao moja walilosawazishia lile la Caen kutoka kwa Nicolas Seube katika awamu ya pili, ambalo Kipa wa Marseille, Steve Mandanda, alishindwa kulihimili.

Olympique lyon pia walionekana kujitahidi katika mashindano hayo na kufanikiwa kutoka sare ya nunge na Monaco.

Paris St Germain ilimaliza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya St Etienne.

Kabla ya kuanza kwa mpabano huo, hata hivyo, palizuka vurumai kutoka kwa mashabiki wa PSG wakipinga mpango wa timu hiyo kuwazuia mashabiki kuchagua viti wanvyokalia wakati wa mechi hiyo.

Mtayarishi :Maryam Dodo Abdalla

Mhariri: Miraji Othman