1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji asitisha kwa muda amri ya marufuku ya rais Trump

Sekione Kitojo
4 Februari 2017

Jaji nchini Marekani jana Ijumaa (03.02.2017)amezuwia kwa muda amri ya rais Trump ya marufuku dhidi ya wasafiri na  wahamiaji kutoka nchi 7 zenye Waislamu wengi, akikubaliana na majimbo 2 yaliyopinga amri hiyo mahakamani

https://p.dw.com/p/2Wxpd
USA Einreiseverbot Trump - Reaktion aus Tokio
Waandamanaji wakipinga amri ya rais TrumpPicha: picture alliance/NurPhoto/R. A. de Guzman

Jaji  wa  wilaya  nchini  Marekani  James Robart  mjini  Seattle alitoa  hukumu  kwamba  majimbo  ya  Washington  na  Minnesota yana  haki  katika   upinzani  dhidi  ya  amri  ya  rais  Trump, ambayo wanasheria  wa  serikali  wanaipinga, na  kusema  inaonekana kwamba  kesi  yao  ina  uwezekano  wa  kufanikiwa.

"Jimbo limekabiliwa  na  mzigo  katika  kuelezea jeraha  ambalo haliwezi  kurekebishwa  kwa  haraka," Robart  alisema. "Amri  hii TRO yaani  amri  ya  muda  wa  kuzuwia, inatolewa  kwa  msingi  wa nchi  nzima.."

USA Präsident Trump - Flugzeug
Rais wa marekani Donald Trump Picha: Reuters/C. Barria

Inafahamika  wazi  mara  moja  kile  ambacho  kinaweza  kutokea baadaye  kwa  watu  ambao  wamesubiri  kwa  miaka  kupata  visa kuja  Marekani.  Idara  ya  usalama  wa  ndani  haikutoa  maelezo, lakini  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  hapo  kabla  iliamuru  kwamba visa  kwa  mataifa  hayo  saba  ziondolewe.

Amri  ya  rais  Trump  wiki  iliyopita  ilizusha  maandamano  nchi nzima  na  mtafaruku  katika  viwanja  vya  ndege  wakati  baadhi  ya wasafiri  walipowekwa  kizuwizini.

USA Trumps Einreiseverbot gestoppt - Generalstaatsanwalt Ferguson
Mwanasheria mkuu wa jimbo la Washington Bob FergusonPicha: Getty Images/K. Ducey

Usalama wa nchi

Ikulu  ya  Marekani ilidai  kwamba  hatua  hiyo  itaifanya  nchi  kuwa salama.

Washington  lilikuwa  jimbo  la  kwanza  kufungua  mashitaka kuhusiana  na  amri  hiyo  ambayo  kwa  muda  inapiga  mafuruku wasafiri  kutoka  Iran, Syria, Sudan, Somalia, Libya  na  Yemen  na kusitisha  mpango  wa  Marekani  wa  wakimbizi.

Mwanasheria  mkuu  wa  jimbo Bob Ferguson  alisema  marufuku hiyo  ya  kusafiri  inaathiri  wakaazi  na  inatoa  nafasi  kwa  ubaguzi. Jimbo  la  Minnesota  lilijiunga  na  mashitaka  hayo  yaliyofunguliwa mahakamani  siku  mbili  baadaye.

Baada  ya  hukumu  hiyo , Ferguson  alisema  watu  kutoka  katika nchi  hizo  zilizoathirika  sasa  wanaweza  kuomba  visa  za  kuingia nchini  Marekani.

"Uamuzi  wa  jaji  Robart , ambao  unaanza  kazi  mara  moja .. unazuwia  amri  ya  rais  Donald Trump  ambayo  ni  kinyume  na katiba na  inakwenda  kinyume  na  sheria," Ferguson  alisema. "Sheria  hiyo  ni  kitu  chenye  nguvu  - ina  uwezo  wa  kumwajibisha yeyote, na  hii  inamjumuisha  pia rais  wa  Marekani."

USA Einreiseverbot Trump - Reaktion der muslimischen Gemeinde
Waislamu wakionesha masikitiko yao nchini Marekani kutokana na amri ya raisPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/R. Chiu

Uwezekano wa rufaa

Gillian M. Christensen , msemaji  wa  wizara  ya  usalama wa  ndani , amesema wizara  hiyo  haitoi  maelezo  kuhusiana  na  suala  lililoko mahakamani. Maamuzi  ya  jaji  yanaweza  kuwekewa  rufaa  katika mahakama  ya  rufaa  ya  9  ya  Marekani.

Amri  ya  jaji  kwa  maandishi, iliyotolewa  jana  Ijumaa , ilisema  sio kazi  ya  mahakama "kuunda  sera  ama  kuamua  busara  ya  sera yoyote iliyotolewa  na  mihimili  mingine  miwili  ya  serikali.

Kazi  ya  mahakama  "ni  kuhakikisha  tu  kwamba  hatua zinazochukuliwa  na  mihimili  mingine  miwili  zinakwenda  sambamba na  sheria  za  nchi."

Robart  aliamuru  washitakiwa  serikali  kuu  " pamoja  na  maafisa wake, mawakala, watumishi, wafanyakazi, wanasheria  na  watu wanaochukua  hatua  kwa  mwongozo  ama  kushiriki  na  serikali wanatakiwa  kwa  pamoja  kuacha " kutekeleza  amri  hiyo  ya  rais.

Idara  ya  forodha  na  ulinzi  wa  mipaka  nchini  Marekani CBP imeyataarifu  makampuni  ya  ndege  nchini  Marekani  kwamba sasa  wanaweza  kuwachukua  wasafiri  ambao  walizuiliwa  na  amri hiyo  ya  rais  wiki  iliyopita, baada  ya kuzuiwa   nchi  nzima siku  ya Ijumaa  na  jaji  mkuu  wa  serikali  katika  jimbo  la  Seattle.

USA Weißes Haus - Sean Spicer
Msemaji wa Ikulu ya marekani White House Sean SpicerPicha: picture-alliance/newscom/UPI Photo/P. Benic

Wakati  huo  huo Ikulu ya  Marekani  jana  Ijumaa (03.02.2017) iliahidi  kupambana  baada  ya  jaji  wa  jimbo  la  Seattle  kuamuru kusitishwa  kwa  muda  amri  ya  kuzuwia  wasafiri  kutoka  nchi saba  za Kiislamu. Msemaji  wa  Ikulu  ya  marekani White House Sean Spicer ameiita  amri  ya  rais  donald Trump "kuwa  ni  sheria ya  sahihi"  na  kusema  wizara  ya  sheria  itaomba  kuzuwia  mara moja  kwa  amri  hiyo  ya  mahakama  ya  shirikisho, mapema iwezekanavyo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo  / ape / rtre

Mhariri :  Zainab Aziz  Mtullya