1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ikulu ya Marekani haijasema lolote juu ya kitabu cha Comey

Amina Mjahid
13 Aprili 2018

Mkurugenzi wa zamani wa shirika la upelelezi la Marekani- FBI James Comey amemshambulia rais wa Marekani Donald Trump na kumueleza kama mtu muovu asiyekuwa na misimamo na asiyekubali ukweli katika kitabu chake kipya.

https://p.dw.com/p/2vz8G
USA Donald Trump und James Comey
Picha: Getty Images/A. Harrer

Katika kitabu hicho kwa jina "A Higher Loyalty," yaani utiifu wa hali ya  juu, Afisa huyo wa zamani wa Shirika la upelelezi FBI James Comey  amemfananisha Trump na Magenge ya wahalifu na kuutaja uongozi wake kuwa ule unaoendeshwa na majivuno au kujionyesha na unaohusu watu kuwa watiifu kwake.

Comey amemuelezea Trump kama mtu aliye ingiwa na shauku mwanzoni mwa utawala wake  kwa kutaka shirika la FBI litupilie mbali  tetesi alizosema sio za ukweli na ambazo zingemtia dhiki mkewe.

USA Anhörung James Comey, früherer FBI-Direktor
Picha: Getty Images/AFP/C. Somodevilla

Katika kitabu hicho kinachotarajiwa kutolewa wiki ijayo,  Comey amefichua taarifa mpya juu ya kukutana kwake na Rais Donald Trump na uamuzi wake mwenyewe wa namna alivyoshughulikia uchunguzi wa barua pepe ya Hillary Clinton kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016.

Amesema Trump ni mhalifu asiyezingatia au kutofautisha kati ya utekelezwaji wa sheria na siasa kwa kujaribu kumshinikiza juu ya uchunguzi wa madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani. Kitabu hicho  kinazungumzia kwa karibu ushuhuda wake na taarifa juu ya mikutano yake na Rais Trump na wasiwasi wake juu ya uadilifu  wa rais huyo wa Marekani.

"Utawala wa rais Trump unahatarisha kile ambacho ni kizuri katika nchi hiii," aliandika Comey  akiuita utawala huo kuwa "moto wa msituni” ambao hauwezi kudhibitiwa na viongozi waliyo na maadili katika serikali ya Trump.

Kundi la sheria la rais Trump kuangalia kwa Umakini kilicho ndani ya kitabu cha Comey

Katika maelezo mengine ya ndani zaidi, Comey ameelezea namna rais Trump alivyoomtaka mara kwa mara kuchunguza madai yaliyomhusu rais huyo na makahaba wa Kirusi wakikojoa kitandani katika hoteli moja nchini Urusi ili athibitishe madai hayo ni ya uwongo.

Trump hata hivyo amekanusha madai hayo lakini Comey anasema inaonekana rais Trump alitaka madai yachunguzwe ili kumridhisha mke wake Melania Trump

USA Donald Trump
Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/E. Vucci

Aidha mwezi Mei mwaka jana Trump alimfuta kazi James Comey hatua iliyoanzisha ushindani katika idara ya haki iliyosababisha Robert Mueller kuteuliwa kuongoza tume maalum inayochunguza madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.

Kitabu hicho kinasemekana kuchunguzwa kwa umakini au kuangaliwa kwa umakini na kundi la sheria la rais Donald Trump, kuangalia makossa yoyote yatakayokuwa yamefanywa kati yake na kiapo alichochukua mbele ya bunge wakati wa uteuzi wake.

Mpaka sasa bado Ikulu ya Marekani haijasema lolote juu ya madai hayo yaliyoandikwa na James Comey katika kitabu chake kinachotarajiwa kutolewa rasmi hadharani wiki ijayo.

Mwandishi Amina Abubakar/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman