1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yajiandaa kwa uchaguzi

Bruce Amani
28 Desemba 2018

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na mtihani mkubwa siku ya Jumapili wakati wananchi watakapopiga kura katika uchaguzi uliocheleweshwa mara kadhaa

https://p.dw.com/p/3AiZX
Kongo Beni | Wahlkampf Emmanuel Ramazani Shadary
Picha: Reuters/S. Mambo

Uchaguzi huo unahitimisha miaka miwili ya vurugu na wasiwasi mkubwa kuwa taifa hilo kubwa kabisa la Afrika ya Kati na ambalo ni tete huenda kwa mara nyingine likatumbukia katika machafuko.

Wagombea 21 wanawania kumrithi Joseph Kabila mwenye umri wa miaka 47 na amekuwa madarakani kwa karibu miaka 18.

Kama kila kitu kitaenda shwari, mshindi ataapishwa Januari 18 – ambapo itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kukabidhi madaraka kwa njia ya amani tangu ilipopata uhuru mwaka wa 1960. Lakini uwezekano wa hilo kufanyika umepungua huku wasiwasi kuhusu uaminifu wa uchaguzi huo ukiongezeka, pamoja na mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Ulaya.

Kongo Beni | Protest & Demonstration gegen Ausschluss von Wahl
Uchaguzi umeahirishwa katika majimbo mawiliPicha: Reuters/S. Mambo

Uchaguzi huo wa rais siku ya Jumapili utakuwa wa kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika miaka saba. Ungepaswa kuandaliwa mwaka wa 2016 wakati Joseph Kabila, aliyeingia madarakani tangu 2001, alipomaliza mihula yake miwili. Lakini alibaki madarakani, na kutengua kipengele cha katiba kilichomhurusu kuendelea kubakia madarakani kwa muda. Hatua hiyo ilisababisha maandamano ya umwagaji damu ambapo watu kadhaa waliuawa. Kisha kukawa na msururu wa kuahirishwa uchaguzi mara tatu – ukifuatiwa na kucheleweshwa kwa mara ya nne wiki iliyopita katika majimbo mawili yanayokabiliwa na machafuko – na mzozo kuhusu matumizi ya mfumo wa upigaji kura kwa njia ya kielektroniki.

Uchaguzi wa rais – utakaofanyika pamoja na wa wabunge na madiwani – una wagombea 21, ambapo watatu wanaongoza katika mstari wa mbele. Wao ni Emmanuel Ramazani Shadary, waziri wa zamani wa mambo ya ndani mwenye msimamo mkali; Felix Tshisekedi, mkuu wa chama kikongwe cha upinzani UDPS; na Martin Fayulu, mbunge asiyekuwa na umaarufu na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya mafuta. Lakini wachambuzi pia wanaeleza kuwepo kwa watu wengine watu wenye nguvu. Majina yao hayapo kwenye makaratasi ya kura, lakini wanaweza kutumia nguvu zao bila kujali atakayeshinda.

Mmoja ni Kabila mwenyewe, ambaye alimteuwa Shadary kuwa mgombea wa chama chake – chaguo ambalo limezusha uvumi wa yeye kurejea katika uchaguzi wa 2023. Wengine ni kiongozi wa zamani wa waasi Jean-Pierre Bemba mwenye umri wa miaka 56 na Moise Katumbi, mwenye umri wa miaka 53, mfanyabiashara tajiri na meya wa zamani wa mkoa wa Katanga.

Viongozi hao wawili walizuiwa kugombea kwenye uchaguzi na wanamuunga mkono kisiri Fayulu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef