1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jammeh akataa kuondoka madarakani

21 Desemba 2016

Rais Yahya Jammeh wa Gambia amesisitiza kutojiuzulu, huku akizikosoa juhudi za upatanishi zinazofanywa na viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambao wanamshauri aondoke madarakani. 

https://p.dw.com/p/2UfBx
Gambias Präsident Yahya Jammeh
Picha: picture-alliance/dpa/S. Zaklin

Jammeh alishindwa katika uchaguzi wa Disemba Mosi na mgombea wa mwanasiasa asiyefahamika sana na aliyeungwa mkono na muungano wa upinzani, Adama Barrow, na kwa mshangao wa wengi akakubali haraka kushindwa huko lakini wiki moja baadaye akabadilisha kauli yake, akidai uchaguzi ulikuwa na kasoro kubwa.

Kwa upande wake, Barrow amejaribu kupunguza hali ya wasiwasi kwa kuahidi kwamba Jammeh hatakabiliwa na mashitaka ya aina yoyote akiondoka madarakani. Mara tu baada ya mgombea wao kutangazwa kuwa mshindi, baadhi ya maafisa wa upinzani walikuwa wametoa kauli zinazoashiria kuwa Rais Jammeh angelikabiliwa na mashitaka kwa ukatili na mauwaji dhidi ya wapinzani wake.

Jammeh anashutumiwa na makundi ya haki za binadamu kwa kuwaweka kizuwizini kuwatesa na kuwauwa wale wanaoshukiwa  kuwa wapinzani katika muda wa uongozi wake wa miaka 22.