1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga jengine la wahamiaji Lampedusa

5 Agosti 2011

Karibu ya wakimbizi 100 kutokea Libya walikufa katika mashua iliosongamana watu na ambayo iliwasili jana katika kiswa cha Italy cha Lampedusa.

https://p.dw.com/p/12Bg6
Karibu watu 100 walikufa katika mashua huko LampedusaPicha: picture alliance/dpa

Watu walionusurika katika mkasa huo walisema wao walikuwa mia tatu katika mashua hiyo, lakini watu mia moja, hasa wanawake hawajanusurika, na wanawaume ilibidi wazitupe maiti hizo baharini. Katika bahari ya Mediterranean sarakasi hiyo ya wakimbizi haionekani mwisho wake.

Baada ya kundi la mwanzo la watu walionusurika kuletwa katika kisiwa cha Lampedusa kilioko Kusini mwa Italy, watu hao walianza kuhadithia kuhusu maafa hayo yaliotokea katika Bahari ya Mediterranean. Mwanamke mmoja aliarifu kwamba watu mia moja, wengi wakiwa ni wanawake, walikufa kutokana na machofu. Na hiyo iliotokana na safari ya wiki nzima kutokea Libya, wakiwa katika mashua ambayo injini yake ilishindwa kufanya kazi. Walinzi wa mwambao wa bahari huko Italy hawajaweza kuhakikisha habari hiyo. Msemaji wa walinzi hao, hata hivyo, alisema kulipatikana nguo za watu majini, na huenda kulikuweko maiti zinazoelea. Lakini utafutaji wa watu ilibidi usimamishwe kutokana na kiza kilichoingia. Nahodha Vittorio Alessandro wa kikosi cha walinzi wa baharini aliiambia redio ya serikali ya Italy:

epa02851511 Italian coast guard officials carry a dead body at a harbour in Lampedusa, Italy, 01 August 2011. According to Italian port authorities, 25 dead bodies were found on a vessel carrying 296 African migrants that set sail from Libya and arrived on Lampedusa early on 01 August. The cause of death was still being investigated. EPA/ELIO DESIDERIO BEST QUALITY AVAILABLE +++(c) dpa - Bildfunk+++
Picha: picture-alliance/dpa

"Ilikuwa operesheni ngumu, kwanza kutokana na umbali mkubwa, kisa hicho kilitokea kilomita 160 kutoka Lampedusa, na kwa upande mwengine kilihusiana na mashua ambayo ilikuwa baharini kwa muda mrefu."

Mashua hiyo iliobeba wakimbizi ilianza safari yake ijumaa iliopita. Kwa jumla, wasaidizi wa kikosi cha walinzi wa baharini waliweza kuwaokoa watu waliokuwa hai kutoka mashua hiyo ilioharibika, na jana jioni watu hao walipelekwa Lampedusa. Wasaidizi hao pia katika mashua hiyo ilioanzia safari yake Libya waligundua maiti. Wengi wa wakimbizi katika mashua hiyo walionekana wamepungukiwa sana maji miilini, kwa masiku hawajanywa maji wala kula chakula. Hamsini kati yao ilibidi wapelekwe kutibiwa katika hospitali ya Lampedusa. Wanawake wawili ni mahututi, na walikuwa wanavuta pumzi kwa kusaidiwa na mashine, huku wakisafirishwa na helikopta kupelekwa Palermo huko Sicily.

Kuna habari kwamba janga hilo angalau lingeweza kuepukwa. Mashua hiyo iliokuweko katika bahari ya Libya iligunduliwa na tishali. Nahodha wa tishali hilo aliwagutusha kwa njia ya dharura polisi wa Italy na akatupa majini vifaa vya uokozi. Kwa mujibu wa shirika la habari la Italy, ANSA, ni kwamba wizara ya mambo ya ndani ya Italy, kutokana na masafa makubwa hadi mahala palipotokea ajali hiyo, iliigutusha kwa njia ya dharura moja kati ya meli za kivita za Jumuiya ya NATO zilizokuwa karibu na hapo na ambazo zinashiriki katika vita vya Libya. Inasemakana NATO ilikataa kufanya operesheni ya uokozi. Hivyo mashua za walinzi wa baharini zikapelekwa kutokea Lampedusa. Jana jioni kutoka wizara ya mambo ya kigeni ya Italy ilitajwa kwamb tuhuma hizo lazima zichunguzwe na NATO. Pindi tuhuma hizo zitadhihirika kuwa ni kweli, basi mkasa huo utakuwa mbaya sana. Katika safari za hatari katika Bahari ya Mediterranean, watu wakiwa katika mshua ndogo,mara nyingi wamekufa. Laura Boldrin, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi:

"Tangu mwisho wa mwezi wa Machi hadi leo, si chini ya watu 1,500 walioanzia safari zao kutokea Libya, kwa bahati mbaya hawajawasili katika upande wa pili wa Bahari ya Mediterranean."

Ni jumatatu iliopita ambapo maiti 25 za watu waliokufa kutokana na kukosa hewa waligunduliwa katika sehemu ya mizigo ya mashua ya uvuvi iliowasili huko Lampedusa. Tangu kuanza uasi wa wananchi katika nchi za Afrika Kaskazini na pia Vita vya Libya zaidi ya watu 45,000 wamekimbia kutoka nchi hizo kupitia bahari ya Mediterranean.

Mwandishi:Troendle, Stefan/Othman, Miraji/ZR/AFP

Mhariri. Mohammed Abdulrahman