1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japani kuwekeza mabilioni Afrika

27 Agosti 2016

Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe ameahidi Jumamosi (27.08.2016) uwekezaji wa dola bilioni 30 kwa maendeleo ya miundo mbinu Afrika katika sekta za taifa na za kibinafsi kwa bara hilo lenye utajiri wa mali asili.

https://p.dw.com/p/1Jr2u
Picha: Reuters/T. Mukoya

Japani nchi ambayo haina rasilmali za asili kwa muda mrefu imekuwa ikiwania kufaidika na utajiri mkubwa wa mali asili barani Afrika kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake ya nishatti hususan baada ya kufungwa kwa muda kwa mtambo wa kuzalisha umeme kwa nguvu za nyuklia wa Fukushima kutokana na ajali.

Abe yuko katika mji mkuu wa Kenya Nairobi kuhudhuria Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Maendeleo ya Afrika (TICAD) ambapo amesema mpango huo wa misaada utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu zikiwemo dola bilioni 10 kwa miradi ya miundo mbinu ambayo itatekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Amewaambia viongozi wa serikali na nchi zaidi ya 30 waliouhudhuria mkutano huo kwamba ukichanganishwa na uwekezaji kutoka sekta binafsi anataraji jumla zitafikia bilioni 30 "huu ni uwekezaji wenye imani na mustakbali wa Afrika,uwekezaji kwa Japani na Afrika kustawi pamoja."

Uwekezaji wa Japani barani Afrika uko kwenye miradi ya barabara,bandari,viwanja vya ndege na mitambo ya umeme.Abe pia amesema uwekezaji huo mpya pia utakwenda kwenye uzalishaji wa ajira na huduma za afya.

Ushawishi wa Japani

Huu ni mkutano wa sita wa kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ambao kwa mara ya kwanza safari hii umefanyika Afrika.

Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mkutano wa (TICAD) Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mkutano wa (TICAD) Nairobi, Kenya.Picha: Reuters/T. Mukoya

Japani tayari imeahidi dola bilioni 32 kwa bara hilo wakati wa mkutano wake uliopita miaka mitatu iliopita.Abe amesema asilimia 67 ya fedha hizo tayari zimeanza kutumika.

Wakati serikali ya Abe imekuwa ikifanikiwa kwa kiasi fulani katika kujiingiza Afrika ushawishi wake umekuwa ukidumazwa na ushawishi wa mpinzani wake China.Hapo mwaka 2015 biashara ya jumla ya China na Afrika ilifikia dola bilioni 179 kwa kulinganishwa na dola bilioni 24 za Japani.

China iliwekeza dola bilioni 2 katika nchi yenye utajiri wa mafuta ya Guinea ya Ikweta katika mwezi wa Aprili pekee mwaka 2015.

Suala la ugaidi

Rais wa Chad na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika Idriss Deby ambaye amehudhuria mkutano huo ameihimiza serikali ya Japani kusaidia katika juhudi za kukabiliana na hali ya kosefu wa usalama kunakosababishwa na kuibuka kwa ugaidi.

Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria katika mkutano wa (TICAD) Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria katika mkutano wa (TICAD) Nairobi, Kenya.Picha: Reuters/T. Mukoya

Amesema katika Mkutano wa Kilele wa hivi karibuni wa Umoja wa Afrika walisema ni muhimu kuiandaa jumuiya ya kimataifa kukabiliana na uovu wote huo.

Amewahamiza washirika wao wote na hususan Japani kuchangia katika Mfuko wa Afrika kupambana na Ugaidi ambao umeanzishwa na mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliofanyika Kigali nchini Rwanda.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Caro Robi