1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je ni ubaguzi uliochochea ugomvi wa Muegln?

P.Martin20 Agosti 2007

Sherehe za mtaani zilizofanywa mwishoni mwa juma lililopita katika mji wa Muegln,mashariki ya Ujerumani,ziliishia kwa ugomvi kati ya wenyeji wa Kijerumani na wafanya biashara wa Kihindi.

https://p.dw.com/p/CHje
Polisi wakiwa na mavazi ya kujikinga katika mji wa Muegln baada ya machafuko yaliotokea Jumamosi usiku kuamkia Jumapili
Polisi wakiwa na mavazi ya kujikinga katika mji wa Muegln baada ya machafuko yaliotokea Jumamosi usiku kuamkia JumapiliPicha: picture-alliance/dpa

Ingawa maafisa katika mji huo hawakutaka kuzungumzia uhalifu uliochochewa na ubaguzi, mashahidi wamesema,ni Wajerumani waliowapiga na kuwafurusha Wahindi,mpaka kikosi kikubwa cha polisi kilipokomesha machafuko hayo.

Polisi wamesema,tamasha la mji wa Muegln lilimalizika kwa ghafula,pale mapigano yalipozuka kati ya wenyeji wa Kijerumani na wafanya biashara wa Kihindi,kwa sababu ambazo hata wachunguzi bado hawazijui.Hata hivyo polisi wanasema,hawawezi kuondosha uwezekano wa kuwepo sababu za kibaguzi, lakini kwanza,wanahitaji kuwapata wale washambulizi kutoka lile kundi la Wajerumani 50. Wahindi walioshambuliwa,walikimbia kujificha ndani ya mkahawa wa Kitaliana ambako walijihami mpaka polisi walipowasili.

Ripoti zingine zinasema,kundi kubwa la wenyeji ama lilisimama na kutazama ugomvi au liliwapigia makofi washambulizi.Polisi wakisema kuwa bado wanahitaji kuchunguza zaidi nani alieanzisha ugomvi huo,mashahidi wameshapitisha uamuzi wao. Mmoja alisema:

“Tulikuwa tukicheza dansi pamoja na Wahindi. Halafu kwa ghafula,wenyeji wachache wa Kijerumani wanaojulikana katika mji wetu kuwa ni wakorofi,walianza kuwashambulia Wahindi.“

Shahidi mwengine akaongezea:

“Wajerumani ndio walianzisha ugomvi.Baadhi ya watu hapa wanadai kuwa ni Wahindi walioanzisha mapigano,lakini huo si ukweli.Yadhihirika kuwa tangu muda mrefu,washambulizi hao walikuwa wakitafuta sababu ya kuwashambulia wageni.“

Mwenyeji mwingine anasema yeye ameshtushwa na tukio hilo.Hataki mji wake kuja kuhusishwa na siasa kali za mrengo wa kulia.

Wakati huo huo Meya Gotthard Deuse wa mji wa Muegln,ana wasi wasi kuwa heba ya mji wake imetiwa doa.Kwa maoni yake vyombo vya habari vinapaswa kuwa na tahadhari vinaporipoti tukio hilo.

Sasa ndio tume maalum ya polisi ipo katika mji wa Muegln kuchunguza kwa makini,sababu halisi za kuwashambulia wananchi 8 wa Kihindi.Kwa mujibu wa mahojiano yaliyofanywa hapo mwanzoni,yasemekana kuwa washambulizi walipaza sauti na kusema „Wageni ondokeni“ na “Hili ni eneo la upinzani wa kizalendo“.

Mazingira kama hayo yanapozingatiwa,yawezekana kuwa mashambulizi yaliyofanywa huenda ikawa yalichochewa na sababu za kibaguzi na si ugomvi uliosababishwa na watu waliolewa chakari.