1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je uchumi wa Ugiriki umeimarika vya kutosha?

Zainab Aziz
20 Agosti 2018

Baada ya miaka mingi ya hatua ngumu za kubana matumizi, Mpango wa tatu wa kuisaidia Ugiriki kuondokana na madeni yake makubwa uliokuwa unatekelezwa na nchi za ukanda wa Euro umemalizika siku ya Jumatatu.

https://p.dw.com/p/33PDC
Belgien EU-Gipfel - Premierminister Alexis Tsipras Griechenland
Picha: Reuters/F. Lenoir

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka minane Ugiriki haitategemea tena msaada wa kifedha kutoka nje. Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz ameiita hatua hiyo kuwa ni ya mafaniko na amesema inatoa ishara kwamba Umoja wa Ulaya una mshikamano.

Kwa jumla Ugiriki ilipokea mkopo wa Euro bilioni 289 kutoka kwa Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Ulaya pamoja na shirika la kimataifa la fedha IMF tangu mwaka 2010, kwa masharti ya kutekeleza hatua kali za kubana matumizi na kuleta mageuzi ikiwa pamoja na kupunguza mishara na malipo ya uzeeni. Kutokana na kukamilika kwa mpango huo Ugiriki imeepuka hatari ya kuondoka kwenye ukanda wa sarafu ya Euro.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amesema baada ya miaka minane ya kukaza mkanda nchi yake leo imefikia ukingoni mwa kitendo cha kupokea misaada ili kuiokoa kifedha kutokana na uchumi wa nchi hiyo kushindwa kunawiri hali iliyoiweka Ugiriki katika hatari ya kuanguka kabisa kiuchumi.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz
Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: picture alliance/dpa/C. Santisteban

Pamoja na kufikia mwisho wa mpango huo wa tatu wa Ugiriki kuokolewa kiuchumi, wasimamizi wa mfuko maalum wa uokoaji wa ukanda wa Euro wameitolea wito nchi hiyo iyafuate masharti yaliyofikiwa kati yake na wakopeshaji.

Mageuzi ya kiuchumi ambayo wakopeshaji walitaka yatimizwe, yalisabisha robo ya thamani ya bidhaa za Ugiriki na pato la jumla la chini hiyo kudorora kwa kipindi cha miaka minane wakati ambapo ukosefu wa ajira uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 27. Maafisa wa Ugiriki wanasema uchumi wa nchi hiyo sasa umerejelea kukua na umeonyesha ziada katika bajeti yake na kiwango cha ukosefu wa ajira kimeshuka na kufikia chini ya asilimia 20.

Mwenyekiti wa bodi inayosimamia utulivu wa Ulaya (ESM) Mario Centeno amesema kwa mara ya kwanza tangu mwanzoni mwa mwaka 2010, Ugiriki sasa inaweza kusimama tena kwa miguu yake.

Amesema haya yamewezekana kutokana na jitihada za watu wa Ugiriki, ushirikiano mzuri na serikali ya Ugiriki ya sasa na msaada wa washirika wa Ulaya kupitia mikopo na kuondolewa kwa baadhi ya madeni.

Profesa wa masuala ya uchumi Nikos Vettas amesema anaamini ni muhimu katika miaka inayokuja kuongeza uzalishaji ili kuupa nguvu zaidi uchumi wa Ugiriki. Hata hivyo Profesa huyo amesema, kaya zilizo katika nafasi dhaifu kutokana na kuathirika kiuchumi katika kipindi cha miaka 10 zitaendelea kuteseka.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga