1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Uingereza inaadhibiwa na Mungu?

Maja Dreyer6 Agosti 2007

Pamoja na yale yanayozingatiwa na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani leo hii ni mripuko wa ugonjwa wa miguu na midomo huko Uingereza na sheria mpya iliyopitishwa Marekani ambayo inaongeza nafasi ya idara za ujasusi kupeleleza juu ya mawasiliano ya watu binafsi.

https://p.dw.com/p/CHSF

Kwanza ni gazeti la “Nordbayrisher Kurier” juu ya ugonjwa wa miguu na midomo ya kifugo nchini Uingereza:

“Baada ya mashambulizi ya kigaidi na mafuriko mabaya, sasa Uingereza inakumbwa na ugonjwa wa wanyama. Ni kama nchi hii inaadhibiwa na Mungu. Miaka sita iliyopita, Uingereza tayari ilikabiliana na mripuko wa ugonjwa wa miguu na midomo ambao uliweza kudhitibiwa baada ya miezi tisa tu. Sasa inabidi kuzuia maafa hayo yasirudiwe.”

Zaidi juu ya ugonjwa wa midomo na miguu ulioripuka Uingereza tunasoma katika gazeti la “Oldenburgische Volkzeitung”:

“Yale yaliyotokea ni kama filamu mbaya juu ya janga kubwa kutokea, yaani chanzo cha virusi vilivyoambukiza wanyama wa shamba la jirani ni maabara ya kampuni ya utafiti ambayo ilitafuta madawa dhidi ya ugonjwa huo huo. Suali ni: Kwa nini maabara hiyo ilijengwa karibu na mashamba ya wanyama? Hiyo haifahamiki, hasa tukikumbuka mripuko mkubwa wa ugonjwa huu mwaka 2001 nchini Uingereza.”

Mhariri wa “Wiesbadener Kurier” anasifu hatua za dharura zilizochukuliwa na serikali ya Uingereza. Ameandika:

“Badala ya kutoa lawama tu, idara husika zinafuata mkakati wa kuzuia ugonjwa kuenea. Matokeo yake yanasaidia pia nje ya Uingereza. Baada ya muda mfupi sana, idara za Ujerumani zilifahamishwa mashamba gani yafungwe kwa sababu yalipelekewa wanyama kutoka Uingereza. Ni ishara ya kwamba kuna mabadilishano ya data juu ya biashara ya wanyama kati ya nchi za Ulaya na idara za serikali zinashirikiana.”

Tuelekee kwenye suala la pili. Nchini Marekani, wajumbe wa mabaraza yote mawili ya bunge, Senate na Baraza la wawakilishi, Congress, waliikubali sheria mpya juu ya kuziruhusu idara za ujasusi kupeleleza mawasiliano ya simu na mtandao wa Internet. Kuhusiana na hayo, gazeti la “Frankfurter Rundschau” limeandika yafuatayo:

“Akitaja tu tarehe 11 Septemba au jina la “Al Qaida” bungeni, rais Bush wa Marekani anaweza kuwashawishi wabunge kukubali sheria kadhaa ambazo zinawatia wasiwasi wanaharakati wa haki za wananchi. Sababu nyingine ni kwamba, wabunge wa Chama cha Demokratik wanahofia kulaumiwa ikiwa hawachukui hatua kali dhidi ya maadui wa demokrasia. Sasa, wapelelezi wa idara za ujasusi wanaweza kusikiliza kisiri mawasiliano yote ya simu ya watu binafsi au kusoma barua pepe ikiwa wanaamini watu hao wanahusika na mambo ya kigaidi.”

Na hatimaye ni gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin. Limeandika:

“Wabunge wa chama cha Demokratic wametoa vipingamizi kadhaa dhidi ya sheria hii mpya, lakini, kimsingi, hakuna hata mbunge mmoja aliyekosoa hatua hii ya kuwapepeleza wananchi. Maana yake ni kwamba katika vita dhidi ya ugaidi, rais wa Marekani anaweza kufanya kila atakalo.”