1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali Babacar Gaye aondoka Syria wakati mzozo ukizidi

Saumu Ramadhani Yusuf25 Agosti 2012

Mkuu wa ujumbe wa waangalizi uliomaliza muda wake Jumapili iliyopita Jenerali Babacar Gaye ameondoka Syria kutokana na kuongezeka kwa mapigano na ukosefu wa nia ya Umoja wa Mataifa kushirikiana kumshinikiza Assad

https://p.dw.com/p/15weC
Jenerali Babacar Gaye
Jenerali Babacar GayePicha: picture-alliance/dpa

Utawala wa Syria bado unaendeleza kampeini yake dhidi ya vikosi vya wapiganaji wa upinzani ambapo wanaharakati wanasema ndege za kivita zinashambulia maeneo ya waasi kaskazini mwa mji wa Aleppo na kuanzisha tena mashambulizi mengine kote nchini humo.

Brahimi aliyechukua nafasi ya mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuhusu mzozo huo wa Syria Kofi Annan amefanya mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Mataifa Ijumaa na kukiri kwamba anahofu juu ya kitisho kinachoukabili ujumbe wake katika kujaribu kuumaliza mzozo huo ulioingia katika mwezi wa 18.

Katibu mkuu wa UN Ban Ki-moon na mjumbe mpya juu ya mzozo wa Syria Lakhdar Brahimi
Katibu mkuu wa UN Ban Ki-moon na mjumbe mpya juu ya mzozo wa Syria Lakhdar BrahimiPicha: picture-alliance/dpa

Mwanadiplomasia huyo mkongwe wa Algeria aliyesimamia mazungumzo ya mwaka 1989 yaliyofikia mwafaka wa kumaliza vita vya Lebanon amesema watatoa kipaumbele katika kuwasaidia wananchi wa Syria kadri wanavyoweza.

Kofi Annan, mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa alimaliza muda wake wa miezi sita wa kujaribu kuleta amani Syria akilalamika juu ya kukosekana juhudi za ushirikiano wa kumfanya rais Bashar al Assad atekeleze mpango wa amani uliopendekezwa.Baraza la kusimamia haki za binadamu nchini Syria Ijumaa lilisema kwamba mwezi huu wa Agosti ndio mwezi mbaya zaidi katika mapigano ya nchi hiyo ambapo watu 4000 wameuwawa ndani ya wiki tatu na kufanya idadi ya watu jumla waliouliwa katika vita hivyo kufikia 24,500:

Mkuu wa jopo la Umoja wa Mataifa la waangalizi jenerali Babacar Gaye ameondoka Damascus Jumamosi baada ya jopo hilo kumaliza rasmi muda wake Jumapili iliyopita wakati vita vikishuhudiwa kuongezeka pamoja na migawanyiko katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa juu ya hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.

President Barack Obama speaks in the White House briefing room, Monday, Aug. 20, 2012, in Washington. (AP Photo/Carolyn Kaster)
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: dapd

Wiki hii serikali ya Syria ilitangaza kuwa tayari kushirikiana na mjumbe mpya wa kimataifa Brahimi na kutaja matumaini kwamba huenda akafungua njia ya kufanyika mdahalo wa kitaifa huku pia ikipendekeza kuwa tayari kuhusu kujadiliana juu ya mpango wa kung'atuka madarakani Assad kama sehemu ya mazungumzo yoyote ya kusaka suluhu.

Nchi za Magharibi zinataka kuushinikiza zaidi utawala wa Assad huku Marekani na Uingereza zikitishia uwezekano wa kupeleka wanajeshi wake kuingilia mgogoro huo ikiwa serikali hiyo ya Syria itatumia silaha zake za Kemikali dhidi ya wapinzani.Ufaransa pia imeunga mkono hatua hiyo ikitaka paweko hatua ya kuzuia ndege za Syria kuruka katika anga ya maeneo fulani nchini humo.

Wanaharakati wanasema Syria imezidisha mashambulizi yake kutokea angani dhidi ya ngome za waasi katika miji ya Aleppo na Damascus.

Mwandishi: Saumu Yusuf

Mhariri Iddi: Ssessanga