1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali Burhan aahidi kuundwa kwa serikali ya kiraia Sudan

Yusra Buwayhid
13 Aprili 2019

Mkuu mpya wa baraza la kijeshi la mpito nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameahidi kufanya mabadiliko ya taasisi za iliyokuwa serikali ya Omar al-Bashir na kuundwa kwa serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3GjFF
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Picha: picture-alliance/AA

Mkuu huyo mpya wa baraza la kijeshi la mpito nchini Sudan ameahidi Jumamosi kufanya mabadiliko ya taasisi za serikali iliyoachwa na rais aliyeondolewa madarakani hivi karibuni Omar al-Bashir, katika hotuba yake ya kitaifa iliyorushwa kwa njia ya televisheni.

"Natangaza kufanya mabadiliko ya taasisi za dola kulingana na sheria na naahidi kupambana na rushwa pamoja na kuuondoa utawala ulipita," amesema Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, siku moja baada ya kuapishwa kama mkuu wa baraza jipya la kijeshi la mpito nchini Sudan.

Burhani amesema wale wote walioshiriki katika mauaji ya waandamanaji watahukumiwa kisheria na ametangaza pia kuondoa marufuku ya kutembea usiku na kuamuru kuachiwa huru kwa watu wote waliofungwa chini ya sheria ya hali ya hatari iliyowekwa na utawala ulioangushwa.

Wakati wa hotuba yake ya kwanza kwa njia ya televisheni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema pia wafungwa wote wa kisiasa wataachiliwa huru. Burhani ameongeza kwamba serikali ya kiraia itaundwa baada ya majadiliano na upinzani a kipindi cha mpito kitadumu kwa muda wa miaka miwili.

Mkuu wa upelelezi ajiuzulu

Awali  Jumamosi, Mkuu wa Idara ya Taifa ya Upelelezi na Usalama, Salah Mohammed Abdallah Salih pia alijiuzulu, kulingana na taarifa ya jeshi. Mkuu huyo wa upelelezi ambaye anajulikana pia kama Salah Gosh, alikuwa kiongozi muhimu wa usalama chini ya uongozi wa al-Bashir.

Wakati huo huo, maelfu ya watu wameandamana nchini Sudan Jumamosi, na kuelekea katika makao makuu ya Jeshi mji mkuu wa Khartoum, baadhi wakiwa katika magari ma wengine wakitembea kwa miguu, wakiendeleza maandamano yanayoendelea kwa muda mrefu na ambayo yamepelekea viongozi wawili kujiuzulu katika kipindi cha siku mbili.

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji mji mkuu wa Sudan, KhartoumPicha: Getty Images/AFP/M. Hemmeaida

Waandamanaji wa Sudan wamesema wanapanga kuendelea kumiminika barabarani hadi pale serikali ya kiraia itakapoingia madarakani.Miezi kadhaa ya maandamano yaliyoongozwa na vyama vya wafanyakazi wa taaluma mbalimbali pamoja na asasi za kiraia yalipelekea kuondolowa madarakani kwa kiongozi wa miaka thelthini Omar al-Bashir.

Watu 16 wauawa wakati wa maandamano

Wakati hayo yakijiri wanaharakati wa Sudan wamesema Jumamosi kwamba watu 16, wakiwamo wanajeshi, wameuawa katika siku mbili za nyuma tangu vikosi vya jeshi kumuondoa madarakano al-Bashir katikati ya maandamano ya kuipinga serikali yake ya miezi kadhaa.

Kamati ya Madaktari ya Sudan, ambayo inahusika na maandalizi ya maandamano hayo, imesema watu 13 wameuawa kwa kupigwa risasi Alhamisi, na watu wengine watatu akiwamo mwanajeshi waliuawa Ijumaa. Kamati hiyo imeelza kwamba walikufa "mikononi mwa vikosi vya utawala na wanamgambo wake."

Abdel Fattah Burhani, mkaguzi mkuu wa vikosi vya majeshi Sudan, aliapishwa kama mkuu mpya wa baraza la mpito la kijeshi, baada ya Ijumaa mkuu wa baraza la mpito la kijeshi Ahmed Awadh Auf alijiuzulu. Hatua hiyo aliitangaza siku moja baada ya kuapishwa katika wadhfa huo ili kuchukua nafasi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo kwa miaka mingi Omar al-Bashir ambaye alikamatwa katika mapinduzi ya kijeshi.

(dpa,ap,afp)