1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali wa kimarekani Irak amuonya al-Sadr

20 Aprili 2008
https://p.dw.com/p/Dl7i

Baghdad:

Jenerali wa majeshi ya Marekani nchini Irak, ametishia hatua kali za kijeshi dhidikiongozi wa kishia mwenye msimamo mkali Moqtada al-Sadr, aliyetoa kitisho kwamba wanamgambo wake wataanzisha mapigano mapya. Meja Jenerali Rick Lynch alisema anataraji al-Sadr hatochochea vurugu na kwamba majeshi yake yako tayari kukabiliana na kiongozi huyo wa kidini, pindi akiamua kupigana. Al-Sadr ameionya serikali ya Irak kutowashambulia wanamgambo wake wa jeshi la Mehd katika eneo la mji wa Baghdad la Sadr ,akiitaka ifuate mkondo wa amani, au iwe tayari kwa vita kamili.

Wakati huo huo watu waliokua na silaha wamewaachia huru wanafunzi wa chuo kikuu waliowateka nyara katika mkoa wa Diyala. Mapema shirika moja la habari nchini humo liliripoti kwamba wanafunzi hao 9 wa chuo kikuu cha Diyala na dereva wao, walitekwa nyara na awatu waliokua na silaha karibu na Baquba, kilomita 57 kaskazini mashariki ya mji mkuu Baghdad. Baquba ni ngome ya wapiganaji wa Kisunni na wanaharakati wa al-Qaeda.