1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeptoo kufika mbele ya tume ya riadha Kenya

9 Januari 2015

Shirikisho la Riadha nchini Kenya AK litaisikiliza kesi inayomkabili Rita Jeptoo Alhamisi wiki ijayo, huku mkimbiaji huyo wa marathon akiamriwa kuhudhuria kikao hicho pamoja na makocha wawili na wakala wake.

https://p.dw.com/p/1EHvD
Chicago Marathon 2013 Rita Jeptoo
Picha: picture-alliance/dpa/Tannen Maury

AK imesema katika taarifa kuwa tume yake ya matibabu na kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu itaendesha kikao hicho katika makao makuu ya shirikisho hilo mjini Nairobi.

Jeptoo, mshindi mara tatu wa Boston Marathon na bingwa mara mbili wa Chicago Marathon, aligundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini nchini Kenya mwezi Septemba. Wiki chache baadaye akashinda taji lake la pili mfulilizo la Chicago.

Alitarajiwa kutangazwa mshindo wa mashindano makuu ya Marathon Ulimwenguni na kupata kitita cha dola 500,000 wakati ilipofichuliwa kuwa vipimo vimeonyesha alitumia dawa zilizopigwa marufuku. Vipimo vya pili vilivyofanywa mwezi uliopita mjini Lausanne katika maabara ya Shirika la Kupambana na Dawa zilizopigwa marufuku Ulimwenguni – WADA viligundua kuwa alitumia dawa hizo.

Jeptoo anakabiliwa na adhabu ya kupigwa marufuku miaka miwili. AK imesema pia imewaita makocha Claudio Berardelli na Noah Busienei, na wakala wa Jeptoo Federico Rosa katika kikao hicho cha Januari 15. Maafisa wa riadha Kenya wanawalaumu makocha wa kigeni na maejenti kwa kuhusika na visa hivyo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reueters/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga