1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Israel yaiomba radhi Ujerumani

30 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCxr

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ameomba radhi kwa sitofahamu iliotokea yenye kuhusisha wanajeshi wa Ujerumani na ndege za Israel nje ya mwambao wa Lebanon.

Maafisa wa serikali ya Ujerumani wamesema ndege za Israel zilishambulia manowari ya Ujerumani kwenye bahari ya kimataifa hapo Jumanne.Israel ilikanusha kwamba ilifyatuwa risasi na kusema kwamba ndege zale zilisogelea manowari hiyo baada ya helikopta kuruka kutoka kwenye meli hiyo bila ya kuvijulisha vikosi vya Israel.

Wakati huo huo serikali ya Ujerumani imethibitisha kwamba haleikopta yake nyengine ilinyemelewa na ndege za Israel hapo Alhamisi usiku lakini hali hiyo haikuwa ya kutisha.

Ujerumani ilichukuwa majukumu ya kukiongoza kikosi cha wanamaji cha Umoja wa Mataifa nje ya pwani ya Lebanon mapema mwezi huu na kazi yake ni kuzuwiya usafirishaji wa silaha wa magendo na kusaidia kudumisha usitishaji wa mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah.