1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM : Rice awasili Israel

1 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBd8

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condolleza Rice amewasili nchini Israel leo hii katika mkondo mpya wa ziara yake Mashariki ya Kati kuweka msingi wa Mkutano wa Kimataifa wa Amani Mashariki ya Kati uliopangwa kufanyika baadae mwaka huu.

Saudi Arabia imekubali kuhudhuria mkutano huo uliopendekezwa na Rais George W. Bush wa Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme Saud al Faisal ametowa tangazo hilo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Jeddah ambao umemshirikisha pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice na waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates.

Saudi Arabia ni mmungaji mkono mkuu wa pendekezo la amani la Umoja wa Waarabu ambalo linaipatia Israel uhusiano kamili wa kibalozi na nchi 22 za Kiarabu ambapo nayo inatakiwa ijitowe katika maeneo ya Waarabu iliyoyakalia kwa mabavu wakati wa vita vya mwaka 1967.

Syria kimsingi imekubali hapo jana kuhudhuria mkutano huo uliopangwa kufanyika mwezi wa Septemba.

Rice leo anatazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert kabla ya kukutana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu Salam Fayyad katika Ukingo wa Magharibi hapo kesho.