1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Watu watatu wakamatwa kwa kujaribu kumkaribia Condoleezza Rice

20 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCQY

Polisi nchini Israel wamewatia mbaroni watetezi watatu waliofaulu hapo jana kuifikia hoteli alimoishi waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice.

Msemaji wa polisi mjini Jerusalem, Micky Rosenfeld, amesema watu hao ni wafuasi wa mtaalamu wa zamani wa ujasusi katika jeshi la Marekani, Jonathan Pollard, aliyehukumiwa kwa kufanya ukachero kwa niaba ya Israel.

Watu hao walipiga kelele wakitaka Pollard aachiliwe huru kabla kukamatwa na walinzi wa waziri Rice. Baadaye polisi waliwaondoa mahala hapo kwenda kuwahoji.

Haikubainika wazi vipi watetezi hao walivyoweza kuikaribia hoteli hiyo. Inaaminiwa kwamba Condoleezza Rice hakuwa katika chumba chake ndani ya hoteli hiyo wakati wa tukio hilo.

Hapo kabla waziri Rice alikutana na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas. Mkutano huo haukufaulu kufikia makubaliano ya kuzifufua juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.