1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi huru la waasi Syria latoa onyo kali kwa Hezbollah

MjahidA21 Februari 2013

Kamanda wa jeshi huru la waasi nchini Syria ameonya kuwa jeshi lake litafanya mashambulizi dhidi ya kundi la Hezbolla nchini Lebanon iwapo hawatokoma kushambulia ngome zinazoshikiliwa na waasi wa Syria.

https://p.dw.com/p/17iem
Wanachama wa Jeshi huru la waasi la Syria
Wanachama wa Jeshi huru la waasi la SyriaPicha: Reuters

Kamanda huyo wa jeshi huru la waasi nchini Syria, Jenerali Selim Idriss, ametoa muda wa saa 48 kwa kundi hilo la Hezbolla kukomesha mashambulizi yake, dhidi ya ngome zinazoshilikwa na waasi la sivyo wanajeshi wake waanze mashambulizi ya moja kwa moja dhidi yao. Kitisho cha Idriss kimetolewa baada ya waasi kuishambulia ndege moja ya serikali na kusababisha makabiliano makali ya kutokea angani yaliosababisha mauaji wa watu 20 mjini Damascus

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Jenerali Selim Idriss amesema kundi la Hezbollah linahujumu utawala wa lebanon kwa kuishambulia Syria hasaa ngome za waasi. Amesema kundi hilo limekuwa kwa muda mrefu likijihusisha na ghasia za Syria lakini kwa sasa limevuka mipaka yake baada ya kuanza kuvishambulia vijiji vilivyo karibu na eneo la Qusayr mjini Homs.

Mpatanishi wa mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi
Mpatanishi wa mgogoro wa Syria Lakhdar BrahimiPicha: AP

Hata hivyo kamanda huyo wa jeshi huru la waasi nchini Syria, Jenerali Selim Idriss, amesema uchokozi wa Hezbolla kamwe hautakubalika na kutangaza kuwa, tayari amemuomba rais na waziri mkuu wa Lebanon kuingilia kati swala hilo, lakini ofisi ya waziri mkuu Najib Mikati imekanusha kuwa na mawasiliano yoyote na waasi wa Syria. Hezbolla imekuwa mara kwa mara ikikanusha kupeleka wapiganaji wake nchini Syria.

Lakhdar Brahimi kurefusha muda wake

Huku hayo yakiarifiwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya nchi za kiarabu juu ya Syria Lakhdar Brahimi anatarajiwa kurefusha muda wake wa kufanya kazi yake hiyo kujaribu kurudisha amani nchini Syria, baada ya takriban miaka miwili ya mapigano. Brahimi anatarajiwa kurefusha muda huo kwa miezi sita ijayo. Muda wake unamalizika rasmi hapo kesho.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey LavrovPicha: AP

Wakati huo huo Urusi na Jumuiya ya nchi za kiarabu zinafanya juhudi za kuwa na mazungumzo kati ya upinzani na serikali nchini Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema wanajaribu kupatanisha pande zote mbili ili kupata amani nchini Syria.

Tangu kuanza kwa mapigano nchini humo takriban watu 70,000 wameuwawa huku wengine wengi wakiachwa bila makao.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa/AP

Mhariri Yusuf Saumu