1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la CRG latoa ripoti ya mauaji ya halaiki Congo

Amina Mjahid 18 Septemba 2017

Ripoti iliyotolewa na kundi la utafiti la Congo imesema makamanda wa jeshi la nchi hiyo walipanga mauaji ya halaiki wakati wakipigania ushawishi mbele ya wanamgambo wanaoipinga serikali Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2kDdL
Demokratische Republik Kongo Beni
Picha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Ripoti hiyo mpya iliyotolewa na kundi la utafiti la CRG la chuo kikuu cha New York  ndio ripoti ya kina na ya hivi karibuni juu ya mauaj ya zaidi ya watu 800, na ya kwanza inayotoa nadharia ya uhakika ya waliyodaiwa kutekeleza matukio hayo.

Ripoti hiyo imeandaliwa kufuatia mahojiano waliofanyiwa watu 249 wakiwemo wahalifu, watu waliyoshuhudia, waathiriwa pamoja na ripoti za ndani za Umoja wa Mataifa na rekodi ya watu waliyokamatwa kuhusika na mauaji hayo.

Inadaiwa milioni kadhaa waliuwawa Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kati ya mwaka 1996 na 2003 katika migogoro ya kikanda huku makundi ya wanamgambo wakiendelea kufanya kazi zao katika maeneo hayo. Lakini mauaji yaliyofanyika mjini Beni ndio yaliyokuwa mabaya na ya kushtua katika matukio ya hivi karibuni.

Wakaazi wakikwepa mashambulizi yaliyokuwa yakifanyika wakati wanajeshi wa serikali wakiingia katika mji jirani wa Goma
Wakaazi wakikwepa mashambulizi yaliyokuwa yakifanyika wakati wanajeshi wa serikali wakiingia katika mji jirani wa GomaPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Kundi hilo la CRG limewanukuu baadhi ya mashahidi waliyosema makamanda wa kijeshi akiwemo aliyekuwa generali mkuu wa kanda hiyo aliunga mkono na hata kupanga mauaji. Katika baadhi ya mauaji hayo duru zimeliambia kundi hilo la CRG kwamba wanajeshi walizingira eneo ili wahanga  wasiweze kutoroka.

Kwa upande wake msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende amesema maafisa kadhaa wa ngazi ya juu tayari wamehukumiwa kufuatia kuhusika katika mauaji hayo lakini pia akaikosoa ripoti ya CRG kwa kujaripu kufufua mambo ya zamani. Hata hivyo jenerali aliyetajwa katika ripoti hiyo Muhindo Akili Mundos,anaendelea kukanusha kuhusika binafsi katika mauaji hayo.

Huku hayo yakiarifiwa ripoti imetoa pendekezo la kufanyika uchunguzi zaidi huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitolewa wito wa kuwawekea vikwazo watu waliyohusika na machafuko yaliyotokea karibu na Beni.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakishika doria Kinshasa
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakishika doria Kinshasa Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompeng

Kulingana na ripoti ya CRG mauaji ya kwanza ya halaiki yalipangwa mwaka wa 2013 na viongozi wa zamani wa jeshi la Congo APC, mrengo wa waasi kutoka vita vya Congo mwaka wa 1998-2003 waliyokuwa wanajaribu kuidhoofisha serikali kuu.

Kwa sasa mauaji makubwa yamepungua Beni mwaka huu lakini wanajeshi kutoka serikali ya Congo na wale wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kupambana na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo. Mmoja ya wanajeshi wa kulinda amani kutoka Tanzania aliuwawa na mwengine kujeruhiwa siku ya Jumapili baada ya mapigano ya wanamgambo. Hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa ujumbe wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa aliyezungumza na chombo cha habari cha Reuters.

Mwandishi:  Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu