1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kuidhinisha azimio kuhusu mzozo wa Burundi

Admin.WagnerD12 Novemba 2015

Baraza la Usalama linatarajiwa kupiga kura leo kuidhinisha kwa kauli moja azimio lililotayarishwa na Ufaransa linalolenga kumaliza machafuko nchini Burundi

https://p.dw.com/p/1H4Mx
Burundi Anschlag in Bujumbura's Ntahangwa
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/Y. Rukundo

Wengi wanahofia huenda yakaongezeka na kuwa mauaji ya watu wengi kama ilivyotokea nchinji Rwanda.

Azimio hilo la Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaanzisha mipango ya Umoja wa Mataifa kuimarisha uwepo wa kimataifa nchini Burundi pengine kwa kuwapeleka wanajeshi wa kulinda amani baada ya kushuhudiwa miezi kadhaa ya machafuko.

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binaadamu wameomba kuchukuliwa hatua dhidi ya kile mashahidi wanakiita kuwa ni ukandamizaji mkubwa wa serikali dhidi ya wapinzani. Kauli zilizotolewa na maafisa wa serikali wiki iliyopita zikirejelea lugha iliyotumiwa katika mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994 nchini Rwanda zimezusha hofu katika Umoja wa Mataifa. Thomas Perriello ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Kanda ya Maziwa Makuu "Serikali ya Marekani ina wasiwasi kuhusiana na machafuko na lugha inayotumiwa na serikali ya Burundi pamoja na ukandamizaji wa vikosi vya usalama na wapinzani wa serikali. Tuna wasiwasi na matumizi ya nguvu kupita kiasi katika pande zote na lugha inayohimiza mgawanyiko, iwe ni wa kisiasa au kikabila. Jamii ya kimataifa inafuatilia kwa makini uchochezi huo"

UN Sicherheitsrat der Vereinten Nationen
Wanajeshi wa MONUSCO huenda wakapelekwa BurundiPicha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Wanadiplomasia wa Ufaransa wanasema wanatarajia rasimu ya azimio hilo kuungwa mkono kwa kauli moja na baraza hilo lenye nchi 15 wanachama. Ufaransa imesambaza rasimu ya azimio ambalo linatinishia kuwawekea vikwazo viongozi wa Burundi ambao wanachochea mashambulizi au kuzuia juhudi za amani.

Azimio hilo litamwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuwasilisha mapendekezo kwa baraza hilo katika siku 15 kuhusu hatua ambazo huenda zikachukuliwa ili kuzuia umwagikaji damu. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanazungumzia mipango ya kuwapeleka haraka Burundi wanajeshi wa kulinda amani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - MONUSCO ikiwa machafuko yatakuwa makubwa kupindukia.

Ujumbe wa MONUSCO nchini Congo una wanajeshi 20,000 pamoja na kikosi kingine cha dharura kinachowajumuisha wanajeshi maalum kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania ambacho huenda pia kikatumwa Burundi ikiwa patakuwa na haja. Aidha Umoja wa Afrika umelitaka Jeshi la Dharura la Afrika Mashariki kuwa tayari wakati kuenda Burundi wakati wowote ikiwa hali itakuwa mbaya zaidi

Burundi imekumbwa na mauaji, mateso na kuzuiwa watu kinyume cha sheria tangu Rais Pierre Nkurunziza alitangaza nia yenye utata ya kuurefusha uongozi wake madarakani mwezi Aprili. Kiasi ya watu 240 wameuawa na wengine zaidi ya 200,000 wamekimbia nchi hiyo

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman